31 July 2013

KIKOSI CHA SIMBA KUKAMILIKA LEO



Na Suleiman Mbuguni
KIKOSI cha timu ya Simba, ambacho kimepiga kambi katika hoteli ya Bamba Beach Kigamboni, Dar es Salaam kujiandaa na Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao, kinatarajia kukamilika leo.Akizungumza Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema wachezaji wao waliokuwa na Taifa Stars, Amri Kiemba na Haruni Chanongo walitarajia kujiunga jana na kambi hiyo.

Alisema wachezaji wengine wa kimataifa, Hamis Tambwe wa Vitalo ya Burundi na Gilbert Kazwe nao wanatarajia kuwasili nchini leo kuungana na wenzao Bamba Beach.“Tunatarajia kwamba kambi ya timu yetu iliyopo chini ya Kocha Mkuu, Abdallah ‘King’ Kibaden na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelu inatarajia kukamilika leo.
  “Na hii ni kutokana na kwamba wachezaji wetu, Amri Kiemba na Chanongo waliokuwa na Taifa Stars walitarajia kujiunga leo jioni (jana), huku wachezaji wa kimataifa nao tunawategemea leo,” alisema.
Kiemba na Chanongo walikuwa na Taifa Stars kwa ajili ya michuano ya kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa Afrika nchini Afrika Kusini, lakini ilitolewa na Uganda kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya kufungwa bao 1-0 jijini Dar es Salaam na wiki iliyopita ilifungwa 3-1 Kampala, Uganda.Kamwaga alisema wachezaji waliopo kambini wanaendelea vizuri na mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na ligi hiyo na pia katika bonanza lao la Simba Day, ambalo hufanyika kila mwaka.

No comments:

Post a Comment