29 January 2013
Wenyeviti waitaka Serikali kuzitambua kazi zao kikatiba
Na Rose Itono
UMOJA wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Dar es Salaam (UWESEMIDA)umeitaka Serikali kuzitambua kazi zao kikatiba kama viongozi wengine kulingana na majukumu yao kikazi.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa UWESEMIDA, Othman Mohamed wakati wa mkutano wao mkuu uliokuwa ukijadili mambo mbalimbali ikiwemo kupitisha rasimu yao kikatiba ili iweze kusajiliwa na kutambulika kikatiba.
Alisema kuwa, kumejengeka tabia ya baadhi ya viongozi wengine kuona kuwa wenyeviti wa serikali za mitaa hawana kazi yeyote kitu ambacho ni ukiukwaji wa taratibu.
Alisema, wenyeviti wa mitaa siku zote ndiyo watendaji wakuu ambao hufanya kazi za kimaendeleo kwa kushirikiana na jamii katika mitaa lakini wamekuwa wakidharaulika.
Mwenyekiti huyo alisema, kulingana na hali hiyo waliamua kuanzisha umoja wao ili kuweza kupashana habari kuhusu fursa mbalimbali zinaweza kutumiwa na wananchi katika kujiletea maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Oysterbay, Peter Mushi alisema kuwa kutokana na hali halisi ya utendaji kazi katika mitaa maofisa watendaji wamekuwa wakijiona ni waungu watu na kuwadharau wenyeviti wa mitaa.
Alisema, hali hiyo inatokana na jinsi serikali inavyowachukulia wenyeviti na kuwaona kuwa ni watu ambao hawana kazi huku wakisahau kuwa kila kitu kinachohusu maendeleo hakiwezi kufanyika ndani ya mtaa pasipo kushirikisha wenyeviti.
Katibu wa UWESEDA, Hassan Kingalu alisema hali hiyo inajidhihirisha na ukweli kuwa serikali haitambui uwepo wa wenyeviti kikatiba mpaka kufikia kutotambua mihuri inayowekwa na wenyeviti katika mitaa.
"Zamani kazi ya mwenyekiti wa mtaa ilikuwa ni pamoja na kuweka mihuri kwa wananchi katika mtaa wake pale linapotokea aidha tatizo au sababu nyingine, lakini sasa hivi wamekuwa hawatambuliki mpaka kuwe na mhuri wa Ofisa Mtendaji,"alisema.
Aliongeza kuwa, hali hiyo inapaswa kutokuwepo na kuwataka maofisa watendaji na wenyeviti kufanya kazi kwa pamoja.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment