08 January 2013

Watatu wafariki matukio tofauti Dar


Na Leah Daudi

WATU watatu wamefariki dunia katika matukio tofauti likiwemo la Nehoma mwenge (25), mkazi wa Tabata Chang'ombe kujinyonga kwa kutumia upande wa khanga kwenye chumba cha shemeji yake.


Akithibitisha  kutokea kwa tukio hilo kamanda wa mkoa wa kipolisi Ilala Marietha Komba alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi katika eneo la Tabata Chang'ombe.

Alisema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa marehemu ni mkazi wa Kigoma alifika Dar es Salaam wiki mbili zilizopita kwa ajili ya kutibiwa mapepo.

Kamanda Komba alisema siku ya tukio mwenyeji wake alikwenda kanisani ndipo alipotumia nafasi hiyo kwa kujinyonga mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali Taifa Muhimbili upelelezi unaendelea.

Wakati huohuo, Ramadhani Khalifani(41) mkazi wa Vingunguti kwa Simba amekutwa chumbani kwake akiwa amejinyonga kwa kutumia waya wa kufungia pazia uliokuwa umetundikwa kwenye dari.

Kamanda Komba alisema kwa mujibu wa maelezo ya mke wake aitwaye Salama Bilali (40), mkazi wa Vingunguti alieleza kuwa marehemu enzi za uhai wake alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa akili kwa muda mrefu.

Alisema marehemu alikuwa akitishia kujiua kwa kujichoma kisu na mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, upelelezi unaendelea.

Katika tukio lingine, mwanaume mmoja aliyetambulika kwa jina la Kayeton Petro (25), mkazi wa Tandika amekutwa amefariki chumbani kwake huku mwili wake ukiwa umelala sakafuni.

Kamanda wa mkoa wa kipolisi Temeke Engelbert Kiondo  alisema  marehemu alikutwa ameshikilia 'Adaptor' kwenye mkono wa kushoto ikiwa wazi jirani na kifua.

Alisema uchunguzi ulibaini kuwa marehemu alikuwa akiunganisha umeme kujaribu kuchaji betri yake ya gari bila kuwa na tahadhari na  kusababisha umeme mkali na alipata majereha mawili makubwa kifuani na mwili umehifadhiwa Hospitali ya Temekle na upelelezi unaendelea.
   

No comments:

Post a Comment