07 January 2013

Moroco adai uchofu umechangia sare na Mtibwa



Na Speciroza Joseph

BAADA ya kutoka sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar, Kocha wa Coastal Union, Hemed Moroco amesema uchovu umechangia kikosi hicho kucheza katika kiwango cha kawaida tofauti na mchezo wake wa kwanza.


Coastal  imetoka sare katika michezo miwili iliyocheza dhidi ya Azam FC na  na Mtibwa sugar na kufikisha pointi 2, nyumba ya Miembeni yenye pointi 3 katika kundi hilo B likiongozwa na Azam FC yenye pointi 4 huku Mtibwa ikiwa ya mwisho kwa kuwa na pointi moja.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo, kocha Moroco alisema uchovu huo umetokana ratiba ya mashindano kucheza kila baada ya siku mbili hali ambayo wachezaji wake hawajaizoea.

Alisema mechi ya mwanzo walikuwa vizuri na kusababisha kutoa ushindani katika mchezo huo, lakini baada ya mechi hiyo walifanya mazoezi mepesi na kucheza mechi kitu ambacho hawakupata muda wa kupumzika.

"Wachezaji walichoka, tutabadilisha aina ya mazoezi kwa kuwa tumegundua tatizo lingine sehemu ya ufungaji, tutafanya mazoezi mengi ya uwanjani ili kupata uzoefu wa kufunga, mechi ya mwisho tutashinda" alisema kocha huyo mwenye asili ya visiwani hapa.

Aliongeza kuwa mashindano hayo yametoa faida kubwa kwa timu yake, amewatambua wachezaji wake hasa wapya waliosajiliwa kwenye usajili wa dirisha dogo mwezi uliopita baada ya kuwatoa wachezaji tisa waliokuwepo katika kikosi hicho.

Timu hiyo leo jioni itamaliza mechi za hatua ya makundi kwa kucheza na Miembeni, Coastal wakishinda wataingia nusu fainali, mechi ya usiku itakuwa kati ya Azam FC na Mtibwa Sugar mechi zote zitachezwa kwenye Uwanja wa Amaan.

No comments:

Post a Comment