11 January 2013

Katiba Mpya izingatie maoni ya TASO



JANA Chama cha Wakulima nchini (TASO), kiliwasilisha maependekezo yake kwa Tume ya Katiba wakitaka Katiba ijayo iondoe migogoro ya ardhi iliyopo kati ya wakulima na wafugaji.


Maoni hayo yaliwasilishwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Engelebeth Moyo, ambaye alisema kuwa, migogoro ya ardhi
kwa makundi inachangia wananchi kupoteza maisha.

Alisema migogoro mingi ya wakulima na wafugaji inachingiwa
kwa kiasi kikubwa na viongozi wa mitaa na vijiji ambao huuza maeneo yanayotumiwa wakulima au wafugaji.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba la Wafugaji, Bw. Daud Haraka, alisema migogoro inayojitokeza kati ya makundi hayo, inatokana
na Serikali kutokuwa na sera madhubuti za mgawanyo wa maeneo.

Sababu nyingine ni kukosekana usimamizi wakutosha kuhusu
ardhi hivyo Katiba ijayo itamke wazi kuhusu sera ya ardhi.

Sisi tunasema kuwa, migogoro ya ardhi nchini imekithiri na kusababisha umwagaji damu. Ni wazi kuwa migogoro mingi inawahusu wakulima na wafugaji.

Migogoro mingine inawahusu wananchi na wawekezaji na kusababisha chuki kwa Serikali. Katika maeneo mengi yaliyohusishwa na migogoro ya ardhi, tayari kumetokea vurugu zilizosababisha uvunjifu wa amani na vifo.

Ni muhimu Katiba ijayo ikamaliza migogoro hii kwa kuyatambua maeneo ya wafughaji na wakulima. Leo hii ni jambo la kawaida kwa watu mbalimbali kujenga eneo analotaka bila kujali la wafugaji au wakulima kwa sababu Serikali haijachukua hatua stahiki ya kutenga maeneo na matumizi yake.

Maofisa ardhi ni miongoni mwa watu wanaochangia migogoro hii kwa kuuza maeneo zaidi ya mara moja hivyo kusababisha jamii kugombana hata kuchukiana.

Sababu kubwa inayochangia maofisa hao kusababisha migogoro ya ardhi ni tamaa ya fedha huku wakijua wanachokifanya ni kinyume na maadili ya kazi zao.

Imani yetu ni kwamba, ardhi ni mali ya mwananchi na Serikali hivyo kila upande unapaswa kushirikishwa wakati wa kuuza au kumtafuta mwekezaji.

No comments:

Post a Comment