11 January 2013

Ghasia aonya tabia chafu ya watumishi kubebana



Na Esther Macha, Mbarali

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bi. Hawa Ghasia, amesema
Serikali imejipanga kukomesha tabia ya baadhi ya watumishi
wa halmashauri kubebwa na baba, shangazi au mama ili
kuongeza kasi ya uwajibikaji sehemu za kazi.

Alisema ni vyema watumishi wakaanza kutumia weledi wao ili kulinda vibarua vyao na kama watashindwa kufanya hivyo, wote watafukuzwa kama itabainika wamefanya uzembe kazini.

Bi. Ghasia aliyasema hayo jana wakati akizungumza na baadhi ya watumishi wa halmashauri mkoani humo ili kuwajengea uwezo
wa kujiwekea mikakati ya kimaadili ya utendaji kazi wao.

“Tabia ya kubekwa kazini kuanzia sasa tutaikomesha, kaa ukijua kama kulikuwa na shangazi yako, mama, baba au binamu ambaye alikuwa anakubeba ujue umekwama na kama ataendelea kukubeba wote mtandoka kwa pamoja,” alisema Bi. Ghasia.

Aliongeza kuwa, kila mtu anatakiwa kulinda kibarua chake hivyo
wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili wasiharibu vibarua vyao na kama watabainika kwa kosa la uzembe watondolewa kazini.

Hata hivyo, aliwataka watumishi hao kufanya kazi kwa masilahi ya
wananchi sio yao binafsi kwani lengo la kuwepo katika idara za Serikali ni kuitumikia jamii na Taifa si vinginevyo.

Bi. Ghasia alisema Serikali haiwezi kuwavumilia watumishi ambao wanafanya kazi zao kwa mazoea na kujigamba wana ndugu wa kuwatetea kama baba, mama, shangazi au binamu.

No comments:

Post a Comment