07 January 2013

Azam kazi ipo leo kwa Mtibwa



Na Speciroza Joseph, Zanzibar

BAADA ya kuwafunga wababe wa Mtibwa Sugar, Miembeni 3-1, timu ya Azam FC leo usiku itashuka Uwanja wa Amaan kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayoendelea visiwani hapa.

Azam FC inaongoza Kundi B kwa kuwa na pointi nne, ikifuatiwa na Miembeni yenye pointi 3, Coastal Union ya tatu ikiwa na pointi 2 huku mabingwa wa zamani wa kombe hilo, Mtibwa Sugar wakiwa wa mwisho na pointi moja.

Mechi za leo kati ya Azam FC na Mtibwa Sugar na Coastal Union itakayocheza dhidi ya Miembeni FC zitatoa picha kamili ya timu zipi zitakazoingia hatua ya nusu fainali kwa kuwa kila timu bado ina nafasi ya kuingia hatua hiyo na kuzirudisha nyumbani timu mbili za mwisho.

Azam FC ikitoka sare aina yoyote na Mtibwa, itaingia nusu fainali, Mtibwa nao wakiifunga Azam FC wataingia huku Coastal kama atahitaji kufuzi lazima imfunge Miembeni wakati Miembeni wao wanatafuta sare aina yoyote ama ushindi kuingia hatua hiyo.

Katika mchezo wa juzi usiku, Azam FC iliipa kipigo cha 3-1 Miembeni, Azam FC walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya pili ya mchezo kupitia kwa beki Jockins Atudo aliyefunga kwa kichwa kutokana na mpira wa kona uliopigwa na kiungo Humphrey Mieno wote kutoka Kenya.

Miembeni walisawazisha bao hilo kupitia kwa mchezaji Adeyum Ahmed aliyepiga mpira wa kona uliokwenda moja kwa moja wavuni, Gaudence Mwaikimba aliiandikia bao la pili Azam FC akipokea krosi ya Mieno na kupiga shuti lililozama wavuni na timu hizo kwenda mapumziko Azam FC ikiwa mbele kwa 2-1.

Kipindi cha pili kilianza huku kila timu zikiwakosa makocha wake Salum Bausi wa Miembeni na Stewart Hall baada ya kutolewa na mwamuzi wa mchezo huo Ally Kisaka kwa kosa la kwenda kumzingira wakati wa mapumziko na makocha hao kuonesha utovu wa nidhamu kwa kujibishana wenyewe kwa wenyewe.

Dakika ya 87 Azam FC walipata bao la tatu lililowekwa na mchezaji Uhuru Selemani aliyeingia dk 60 kuchukua kua nafasi ya Khamis Mcha, Uhuru alitumia vyema mpira uliorudi baada ya beki wa Miembeni kuokoa vibaya shuti la Mwaikimba, Uhuru alipiga shuti likatinga wavuni na kumaliza mchezo Azam FC ikishinda 3-1.

Katika mchezo wa jioni, Coastal Union ilitoka sare 1-1 na Mtibwa Sugar katika uwanja huo, Mtibwa walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 58 lililowekwa wavuni na Ally Mohamed aliyepiga shuti likagonga mwamba na kuingia wavuni.

Coastal walisawazisha dakika ya 81 kupitia kwa nahodha Jerry Santo aliyepiga shuti la mbali lililopita moja kwa moja wavuni akimalizia krosi ya Mohamed Soud, katika mchezo huo Mtibwa ilicheza pungufu baada ya nahodha wake Salum Swedi kutolewa kwa kadi nyekuwa akiwa ameoneshwa kadi mbili za njano na mwamuzi Waziri Sheha.

Baada ya michezo ya leo, nusu fainali ya kwanza itachezwa Jumatano na ya pili Alhamisi wakati fainali itapigwa Jumamosi ambapo ni kilele cha sherehe za kuadhimisha miaka 49 ya Mapinduzi Zanzibar.

No comments:

Post a Comment