07 January 2013
Serikali yataka vyama viige kwa TTA
Na Zahoro Mlanzi
VYAMA mbalimbali vya michezo nchini vimetakiwa kukiiga Chama Cha Tenisi Tanzania (TTA) kwa kuwekeza zaidi kwa vijana ili kuliletea manufaa taifa na kukuza michezo nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa michuano ya ubingwa wa tenisi kwa Vijana kwa nchi za Afrika Mashariki yaliyoandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Tenisi (ITF) na lile la Afrika (CAT), Naibu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Juliana Yassoda alisema kwa sasa ni TTA pekee wanaowaandaa vijana kimichezo na kuandaa mashindano yao ya kimataifa.
Alisema vijana 62 kutoka Kenya, Sudan, Ethiopia, Djibouti, Rwanda, Burundi na wenyeji Tanzania wanashiriki mashindano hayo ya wiki moja yaliyodhaminiwa na Kampuni ya Saruji Tanga kupitia bidhaa yake ya Simba Cement.
“Ni fahari kwa serikali kushuhudia vijana wakishiriki mashindano haya makubwa ya ukanda wa Afrika Mashariki chini ya udhamini wa Simba Cement, lakini tungependa wadhamini zaidi wajitokeze na kuachana na ile dhana potofu ya kuwekeza kwenye soka pekee. Ni fahari pia kufahamu kuwa TTA wao hawanunui wachezaji kutoka nje, bali wanawekeza kwa vijana na ndio hawa ambao leo wanaiwakilisha nchi yetu,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa TTA, Inger Njau alisema michuano hiyo itatumika kuwapata wachezaji watakaoshiriki katika michuano ya Afrika kwa vijana itakayofanyika Nairobi, Kenya Machi, mwaka huu.
“Tunatarajia kuwa wachiriki wataitumia michuano hii ya Dar es Salaam kuimarisha viwango vyao na kujiweka tayari kwa michuano itakayofuata,” aliwaambia makocha na wachezaji hao kutoka nchi saba waIiokusanyika kwenye viwanja vya Klabu ya Gymkhana, Dar es Salaam (DGC).
Pia Ofisa Mawasiliano wa Simba Cement, Mtanga Noor alisema kampuni hiyo imejitolea kuwekeza kwa vijana na imeyadhamini mashindano hayo kwa karibu sh. milioni 21.
“Watanzania wanapaswa kufahamu kuwa ipo pia michezo mingine maarufu mbali na soka na ndio maana mwaka jana tulimleta nchini mchezaji namba moja wa tenisi duniani ili kuwahamasisha vijana,” alisema Noor.
Katika mechi za ufunguzi, Mtanzania Asia Morris alifungwa na Mariam Mujawimamu kutoka Burundi kwa seti 2-0, wakati Abdul Kabura wa Burundi akicheza na Halfan Peter wa Tanzania.
Mechi nyingine zilikuwa ni kati ya Grace Pancras na Rahabu Shaban wote kutoka Tanzania na Diella Syori kutoka Burundi aliyecheza na Peggy Musuku.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment