01 August 2012
Ngorongoro Heroes, Nigeria zaingiza mil. 12/-
Na Amina Athuman
MECHI ya kwanza ya raundi ya pili kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 kati ya Tanzania (Ngorongoro Heroes) na Nigeria (Flying Eagles) iliyochezwa Julai 29 mwaka huu imeingiza sh. 12,901,000.
Akizungumza Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 3,377 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo lililochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Alisema Sehemu iliyoingiza watazamaji wengi ilikuwa viti vya bluu na kijani ambapo 2,697 walikata tiketi kwa kiingilio cha sh. 3,000 kila mmoja. Viingilio vingine katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B, na sh. 15,000 kwa VIP A iliyoingiza watazamaji 21.
Wambura alisema mgawanyo wa mapato hayo ni kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ilikuwa sh. 1,967,949.15, gharama ya kuchapa tiketi sh. 2,250,000, gharama za waamuzi na kamishna wa mechi hiyo sh. 760,000 na ulinzi na usafi kwa Uwanja wa Taifa sh. 2,350,000.
Alisema malipo kwa Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000, asilimia 20 ya gharama za mchezo ni sh. 714,610.17, asilimia 10 ya uwanja sh. 357,305.08, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 178,652.54 na asilimia 65 ya TFF sh. 2,322,483.05.
Ofisa huyo alisema mechi ya marudiano ya michuano hiyo ambayo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Algeria itachezwa Agosti 12 mwaka mjini Ilorin, Jimbo la Kwara, Nigeria.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment