26 July 2012

Yanga, APR gharika leo Kagame



Na Elizabeth Mayemba

MABINGWA watetezi wa Kombe la Kagame Yanga leo wanashuka uwanjani kumenyana na APR ya Rwanda katika nusu fainali ya michuano hiyo ya Kagame, mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Taifa kuanzia saa 10 jioni.

Kabla ya mchezo huo ambao unatarajiwa kujaza mashabiki wengi wa soka nchini, mechi ya kwanza itawakutanisha wawakilishi wengine wa Tanzania katika michuano hiyo Azam FC ambao watamenyana na AS Vita ya Kongo, mechi ya nusu fainali ya kwanza itakayoanza saa 8 mchana kwenye Uwanja huo.

Yanga walifanikiwa kutinga hatua hiyo baada ya kuwafungashia virago Mafunzo ya Zanzibar kwa mikwaju ya penalti 5-4, huku Azam FC wakiwaangushia kipigo kikali mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba kwa mabao 3-1.

Akizungumzia mechi hiyo Kocha Mkuu wa Yanga Tom Saintief alisema ni mechi ngumu hivyo wanatakiwa kucheza kufa au kupona ili waweze kutinga fainali ya michuano hiyo.

"Endapo tutaingia fainali basi bila shaka tutatetea ubingwa wetu kwani hilo ndilo nililokuwa nikiliomba siku zote, hivyo wachezaji wangu wanatakiwa kuwa makini sana," alisema Tom.

Alisema pia wachezaji wake wasije wakajifariji kwa mechi ya kwanza ambayo waliifunga APR kwa mabao 2-0 kwani mechi ile APR na wao walikuwa wanacheza ili kukamilisha ratiba tu kwani zote zilikuwa tayari zimeshapita.

Tom alisema wachezaji wake wanaendelea vizuri na mazoezi akiwemo kipa wao Yaw Berko ambaye anakabiliwa na majeraha ya goti, hivyo uwezekano wa kucheza bado hana uhakika mpaka daktari atakaporidhika na hali yake.


Kwa upande wa Azam FC Kocha Mkuu wa timu hiyo Stewart Hall alisema anashukuru kwa timu yake kuingia katika hatua muhimu kama hii, hivyo wanachangamoto kubwa kuhakikisha pia wanaingia fainali.

"Hatua tuliyofikia ni ngumu mno lakini muhimu ni wachezaji wangu kujua wanafanya nini uwanjani ili tuweze kutinga fainali, Vita ni timu kubwa ambayo tangu awali ilionesha upinzani mkali sana," alisema Hall.

Katika mechi za leo viingilio kwa VIP A ni sh.20,000, VIP B sh.15,000, VIP C sh.7,000 na viti vilivyobakia kiingilio ni sh.5,000.

No comments:

Post a Comment