26 July 2012
Mkutano Mkuu Simba Agosti 5 *TBL yawapa sh.milioni 20
Na Zahoro Mlanzi
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro Lager jana ilikabidhi hundi ya sh.milioni 20 kwa klabu ya Simba kwa ajili ya Mkutano wake Mkuu unaotarajiwa kufanyika Agosti 5, mwaka huu.
Akikabidhi hundi hiyo Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema wakiwa kama wadhamini wa timu za Simba na Yanga wanatambua wajibu wao na wana nia ya dhati ya kuendeleza soka nchini.
“Kilimanjaro Premium Lager inatambua wajibu wake na ina nia ya dhati kuendeleza soka nchini na kwa kuzingatia hilo tungependa kuona maendeleo ya Simba na ndio maana tunaiunga mkono klabu hii katika mkutano wake mkuu,|" alisema Kavishe.
alisema wanaamini kuwa mkutano huo utaimarisha uhusiano uliopo kati ya klabu na wanachama wake kwa kuwapa fursa ya kuhakiki mwelekeo wa klabu yao waipendayo.
“Mtu anapoangalia historia ya klabu hii kongwe ambayo imejengeka kutokana na rekodi nzuri ya mafanikio kwa muda mrefu utaona kwamba ina mamilioni ya wapenzi nchini. Soka ndio ndio mchezo mkubwa zaidi hapa Tanzania na bia ya Kilimanjaro imekuwa ikitoa mchango mkubwa kusaidia mchezo huu na ndio maana tunasaidia mkutano mkuu wa Simba ili kusaidia kudumisha uwajibikaji wa klabu kwa wanachama wake.
“Tunatambua wajibu wetu kama wadhamini wakuu wa Simba katika kutekeleza mkataba wetu, tutaendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha tunalipeleka soka la Tanzania kwenye kilele cha mafanikio," alisema Kavishe.
Naye Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu', aliishukuru kampuni hiyo kwa kuendelea kutekeleza makubaliano ya mkataba wao.
Alisema fedha hizo zitatumika katika mkutano huo ambao utafanyika kwenye Bwalo la Polisi Officers Mess Oysterbay na kwamba utaanza saa nne asubuhi, hivyo wanachama wote wahakikishe kadi zao ni hai.
Alisema katika mkutano huo watazungumzia mapato na matumizi ya mwaka jana pamoja na kupitisha bajeti mpya ya mwaka huu ili wapate mwanga wa kutumia fedha zao.
Alisema pia siku hiyo watazindua Wiki ya Jamii ambapo siku inayofuata baada ya mkutano watatembelea Kituo cha Watoto Yatima cha Mango na Agosti 7, watatembelea wagonjwa katika hospitali ya Mwananyamala.
"Agosti 8 tutakuwa na Simba Day ambapo siku hiyo tutacheza mechi moja ya kimataifa, Agosti 9 tutatembelea Shule ya Msingi Mgulani ambapo tutakwenda kuhamasisha michezo na tutahitisha wiki hiyo ya jamii kwa kutembelea TBL na kujionea mambo mbalimbali," alisema Kaburu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment