26 July 2012

Wadau: Uwanja wa Majimaji unatia kichefuchefu



Na Mhaiki Andrew, Songea

WAPENZI na mashabiki wa soka mkoani Ruvuma wamelalamikia ubovu wa uwanja wa Majimaji kutokana na wamiliki wake ambao ni Chama chaMapinduzi(CCM), kushindwa kuufanyia matengenezo huku wakiendelea kuchukua ushuru wa uwanja huo na pango la vyumba vya uwanja kila mwezi.

Wakizungumza mjini hapa kwa nyakati tofauti juzi, baadhi ya wadau na wapenzi wa soka walisema kuwa hali hiyo ya ubovu wa uwanja endapo hakutafanyika ukarabati huenda hata mechi za Ligi ya Taifa ya Daraja la kwanza zikachezwa nje ya mkoa kama Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wataliona hilo.

Walisema hali hiyo imekuwa ikichangia kushuka kwa viwango vya soka kwa wachezaji ambao wamekuwa wakicheza kwa uoga kwa kuogopa kuumia kama watacheza kwa kujituma na hivyo kuishia kupewa lawama kwa mashabiki wao pale timu inapofungwa.

Mmoja wa wadau hao, Mohamed Mchele alisema wamiliki wa uwanja huo ambao ni chama cha Mapinduzi(CCM) wameshindwa kuufanyia ukarabati uwanja huo ambao umekuwa moja ya viwanja maarufu hapa nchini kama ile ya Taifa,Dar es Salaam, CCM Kirumba(Mwanza) na Nangwanda (Mtwara).

Alisema katika kuliona hilo ameshauri wadau wajitokeze kuchangia fedha  ambazo zitasaidia kuufanyia ukarabati uwanja huo kwa kujaza kifusi cha mchanga pamoja na kumwagiliaji maji, ili kuokoa  timu zao za Majimaji na Mlale JKT ambazo zinashiriki ligi  ya Taifa ya Daraja la Tatu msimu huu.

Alisema pamoja na michango hiyo ya fedha ambazo zitalenga kuufanyia ukarabati  uwanja huo, pia utasaidia kutoa fursa kwa wapenzi na mashabiki kuendelea kuzishuhudia timu zao zikicheza katika uwanja huo, ambao tayari umepoteza umaarufu ikilinganishwa na miaka ya nyuma enzi za muasisi wake, marehemu Dkt Lawrence Mutazama Gama, ambapo uwanja ulikuwa katika hali ya ubora ikiwemo na miundo mbinu ya maji safi katika maeneo yake yote na maji taka.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha soka, Manispaa ya Songea(SUFA), Godfrey Mvula alipoulizwa juu ya uwanja huo  alishangazwa na CCM kung'ang'ania kumiliki uwanja huo wakati uwezo wa kuuhudumia hawana, huku wakiendelea kukusanya pango la vyumba na ushuru wa uwanja kwa kila mechi kwa kuchukua asilimia 10 ya fedha za viingilio vya milangoni.

Alisema hatua iliyochukuliwa na wadau wa soka ya kuhamasisha kuchangia fedha kwa lengo la kuufanyia ukarabati uwanja utasaidia kunusuru TFF kuzipeleka mechi za Majimaji na Mlale JKT kuchezwa kwenye viwanja nje ya mkoa kwa sababu ya tatizo la ubovu wa uwanja.


Hata hivyo juhudi za kumpata Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Verena Shumbusha ziligonga mwamba baada ya kudaiwa na wahudumu wake kuwa hakuwepo ofisini kwake.

No comments:

Post a Comment