26 July 2012
Mchumiatumbo kuzichapa na Zola D Idd El Fitri
Na Peter Mwenda
MABONDIA Alphonce Joseph (Mchumiatumbo) na David Michael Mlope (Zola D – King) watapambana katika Tamasha la Watani wa Jadi litakalofanyika katika Sikukuu ya Idd El Fitri kwenye Uwanja wa Chuo cha Bandari Temeke.
Mwenyekiti wa SHIWATA, Cassim Taalib alisema tamasha hilo ni kwa ajili ya kukusanya fedha za Ujenzi wa nyumba za kisasa za gharama nafuu kwa ajili ya Wasanii, Waandishi wa Habari na Wanamichezo katika Kijiji cha Mwanzega, Mkuranga.
Alisema Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) ndio wanaosimamia pambano hilo la Mabondia hawa watakaocheza katika uzani wa juu (Heavy weight) raundi nane (8) pia kutakuwa na pambano moja la utangulizi.
Taalib alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Viwango vya mabondia wa kulipwa wa TPBC, Boniface Wambura ametoa kibali cha pambano hilo wakati wa Sikukuu za Iddi el fitri, Agosti, 2012.
Alisema pamoja na pambano hilo, kutakuwa na mechi ya mpira wa miguu kati ya Simba na Yanga (Veteran) katika Uwanja huo huo wa Chuo cha Bandari Temeke na mshindi wa mchezo huo atazawadiwa ng’ombe dume.
Taalib alisema kwamba kikundi cha Mchiriku cha Jagwa kitatumbuiza, Roman Mg’ande wa Msondo atapigana mieleka na Lumole Matovolwa (Big) na upande wa wanawake Sophia Lubuva wa Simba atapambana na Mwajuma Jimama wa Yanga huku washangiliaji wa Mpira Pesa (Simba) watapambana katika mpira wa miguu na Watani wao wa jadi Yanga Bomba.
Alisema tamasha hilo pia litapambwa na mechi ya mpira wa kikapu ya Ngongoti pamoja na mashindano ya pikipiki ambayo yanatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa watoto na wakubwa ambao siku hiyo watakuwa wakisherekea Sikukuu ya Idd el Fitri baada ya kumalizika kwa mwezi wa Ramadhani, Wasanii wa Bongo Flava nao watakuwepo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment