26 July 2012

Mil. 56.3/- zatengwa kukamilisha miundombinu shule za sekondari


WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imesema mwaka wa fedha 2012/13, Serikali kupitia Mpango wa Elimu ya Sekondari (MMES II), imetenga sh. bilioni 56.3, kwa ajili ya kukamilisha  miundombinu ya shule 264.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Bw. Philipo Mulugo, aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Bi. Susan Lyimo (CHADEMA).


Katika swali lake, Bi. Lyimo alitaka kujua Serikali inazungumziaje suala zima la upungufu wa vitendea kazi katika shule nyingi nchini.

Akijibu swali hilo, Bw. Mulugo alisema Serikali imetenga sh. bilioni 56.3, kwa ajili ya ujenzi wa maabara, maktaba, madarasa, nyumba za walimu, vyoo na kuweka umeme.

Alisema Serikali pia inawaelekeza wakuu wa shule husika kutumia asilimia 50 ya fedha za ruzuku ya uendeshaji kununulia vifaa kama vitabu na kemikali kwa ajili ya maabara za sekondari.

Aliongeza kuwa, pia Serikali imekuwa ikikabiliana na changamoto ya upungufu wa vitendea kazi kadiri hali ya fedha inavyoruhusu.

“Mwaka wa fedha 2011/12, Serikali ilipeleka fedha katika mamlaka za Serikali za Mitaa sh. bilioni 20.8 ili kuboresha miundombinu kwenye shule za sekondari.

“Fedha hizi pia zimelenga kufanya ukarabati wa shule kongwe 63 kwa gharama ya sh. bilioni 3.2, ununuzi wa maabara ambazo zinahamishika kwa ghrama ya sh. bilioni tatu pamoja na ujenzi wa hosteli sh. bilioni 14.6,” alisema Bw. Mulugo.

Akizungumzia suala la ulipaji madeni  ya walimu, Bw. Mulugo alisema suala hilo limekuwa na changamoto kubwa za ulipaji wa madeni hayo kutokana na baadhi ya walimu kuchelea kutuma madai yao hivyo kulazimika kusubiri mwaka wa fedha unaofuata.

Changamoto nyingine ni baadhi ya walimu kutowasilisha vielelezo muhimu kama fomu za madai, stakabadhi, tiketi, hati za kuzaliwa, hati za ndoa na baadhi ya vielelezo kuwa na dosari.

No comments:

Post a Comment