26 July 2012

Walimu wadanganyifu katika mitihani kuchukuliwa hatua




SERIKALI imetangaza kuchukua hatua za kisheria kwa walimu ambao wanajihusisha na vitendo vya udanganyifu wa matokeo ya mitihani ya darasa la saba.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bw. Philipo Mulugo, aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Ngara, Bw. Deogratiaa Ntukamazina (CCM).

Alisema mbali ya udanganyifu uliofanywa na walimu katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2011, zipo taarifa kuwa katika Mkoa wa Mwanza, lipo tatizo la udanganyifu na kudai atahakikisha walimu hao wanachukuliwa hatua kama ilivyokuwa mkoani Kigoma hivi karibuni.

Katika swali lake la msingi, Bw. Ntukamazima alitaaka kujua ni lini Serikali itaipatia Idara ya Elimu fedha za mafuta ili shule nyingi ziweze kufanyiwa ukaguzi kwani hivi sasa hazifanyiwi ndio maana wanafunzi wengi wanafaulishwa kwenda sekondari bila kujua kusoma na kuandika.

Bw. Mulugo alisema, hivi sasa shule za msingi zinafikia 16,000 na sekondari 4,367 jambo ambalo Serikali imebaini kuwepo kwa kasoro katika idara hiyo ya ukaguzi.

“Wizara yangu itaendelea kutenga na kutoa fedha kwa ajili ya ukaguzi wa shule hizo kadri ya upatikanaji wa fedha kutoka hazina, pia tumeandaa andiko ambalo litaiwezesha idara  hiyo kuwa wakala ili kuimarisha shuguli za ukaguzi,” alisema Bw. Mulugo.


No comments:

Post a Comment