26 July 2012
Japan imetoa msaada kubwa wa mchele nchini - Serikali
SERIKALI ya Japan, imekuwa ikitoa msaada wa mchele kwa Tanzania tangu mwaka 1979.
Kwa mjibu wa takwimu zilizopo toka mwaka 1992 hadi 2011, mchele uliotolewa na Japani ni tani 183,366.92, sawa na fedha za Kijapan bilioni 7.770.
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Adam Malima, aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Konde, Bw. Katib Said Haji (CUF).
Katika swali lake, Bw. Haji alitaka kujua msaada wa Japan kwa Tanzania ulianza kutolewa mwaka gani na thamani yake umefikia kiasi gani cha fedha na Zanzibar ulianza kupelekwa lini.
Akijibu swali hilo, Bw. Malima alisema kati ya mwaka 1979 na 1990, mchele wa msaada kutoka nchini Japani ulipokelewa na kusambazwa na Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC).
Alisema mwaka 1991 na 1995, Kampuni ya Bishara la Consumer Service ambayo awali lilikuwa Shirika la Umma, pia ilipokea mchele wa msaada na kuuuza kwa niaba ya Serikali.
Aliongeza kuwa, utaratibu wa kuipa Tanzania Zanzibar mgawo wa chakula hicho, ulianza mwaka 1995 ambapo tani zilizopelekwa hadi mwaka 2011 zilikuwa 7,218.98.
“Mwaka 1999 na 2005, hakukuwa na mgawo rasmi kwa Zanzibar ambapo mchele uliopokelewa kwa kipindi hicho uliuzwa kwa utaratibu wa zabuni ya wazi.
“Kampuni yoyote kutoka katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliruhusiwa kuomba zabuni ya kununua na kusambaza, Serikali iliuza mchele huu kwa mkopo lakini baadhi ya kampuni zilishindwa kurejesha fedha zote za mauzo,” alisema.
Aliongeza kuwa, baada ya Serikali kuchoka kufuatilia madeni hayo iliingia mkataba na kampuni ya kukusanya madeni ya Msolopa Investment Company ambayo inaendelea na kazi hiyo hadi sasa.
Alisema hivi sasa zipo kampuni nane ambazo zinadaiwa fedha za kusambaza mchele huo na zingine za umma ambazo tayari zilishakufa lakini Serikali itaendelea kutumia vizuri fursa ya msaada wa mchele kutoka Japani kwa manufaa ya Watanzania.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment