08 May 2012

Taifa Queens, Lesotho kazi moja leo Kombe la Afrika



Na Amina Athumani

TIMU ya Taifa ya netiboli (Taifa Queens), leo itafungua pazia la michuano ya Kombe la Afrika kwa kuumana na Lesotho katika mchezo utakaopigwa saa nane mchana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kabla ya mchezo huo utatanguliwa na mchezo kati ya Botswana itakayomenyana na Malawi ambapo mchezo huo nao utachezwa kwenye uwanja huo huo.


Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Netoboli Tanzania (CHANETA), Rose MKisi alisema maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo imekamilika.

Alisema timu zote nane zimeshawasili kwa ajili ya michuano hiyo itakayofunguliwa na Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Salma Kikwete.

Alisema tayari viongozi mbalimbali kutoka Shirikisho la Netiboli Duniani (IFNA) pamoja na waamuzi mbalimbali watakaochezesha michuano hiyo wamewasili.

Alisema ratiba nyingine ya michuano hiyo itatolewa leo mara baada ya ufunguzi zitakazopambwa na nyimbo za mataifa mbalimbali yanayoshiriki michuano hiyo kwa kupigwa kwa blast band.

Alisema kwa upande wa Taifa Queens ipo kwenye ari ya ushindani na kwamba makocha wote kutoka Bara na Zanzibar wamejipanga kuhakikisha timu hiyo inaaza vema michuano hiyo.

Taifa Queens inaundwa na Pili Peter, Irene Elias, Beth Kazinja, Jacqueline Skozi, Restuta Boniface, Doritha Mbuta na Lilian Sylidion.

Wengine ni Matalena Muhagama, Paskalia Kibayasa, Siwa Juma, Subira Juma, Subira Songwe, Penina Mayunga, Evodia Kazinja, Niza Nyange, Mwanaid Hassan, Lydia Samwel na Joyce Edward.

Michuano hiyo itafikia kilele chake Mei 12, mwaka huu ambapo hii ni mara ya pili kufanyika kwa michuano hiyo ambapo mara ya kwanza ilifanyika 2009.

Michuano hiyo itaiwezesha Tanzania kupanda viwango vya Dunia vya IFNA ambapo kwa sasa Tanzania ipo nafasi ya 20.



No comments:

Post a Comment