08 May 2012

Lulu aombewa ashtakiwe mahakama ya watoto



Na Rehema Mohamed

MAWAKILI upande wa utetezi katika kesi inayomkabili msanii maarufu nchini, Elizabert Michael 'Lulu', wamewasilisha mahakamani ombi la kutaka mahakama hiyo imuone mshtakiwa huyo ana miaka chini ya 18 hivyo kesi hiyo ihamishiwe katika mahakama ya watoto.

Ombi hilo liliwasilishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana na mmoja wa mawakili wanaomtetea Lulu, Kened Fungamtama mbele ya Hakimu, Agustina Mmbando wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Wakati Fungamtama akiwakilisha ombi hilo, aliiambia mahakama hiyo kuwa mshtakiwa huyo ana miaka 17, hivyo shauri lake linatakiwa kuhamishiwa katika mahakama ya watoto.

Aliongeza kuwa upande wa mashtaka haujawasilisha mahakamani hapo pingamizi lolote kuhusu umri wa miaka hiyo hata pale mshtakiwa mwenyewe alipoieleza mahakama kuwa ana miaka 17 badala ya 18.

Katika kuunga mkono ombi hilo Fungamtama aliwasilisha cheti cha kuzaliwa  alichodai kuwa cha mshtakiwa ili mahakama hiyo iweze kujiridhisha kuhusu umri wa mshtakiwa huyo kinachoonesha mwaka na mahali alipozaliwa.

Hata hivyo wakili wa serikali katika kesi hiyo, Elizabert Kaganda alipinga ombi hilo na kudai kuwa ameshtushwa na ombi hilo kwakuwa kesi imekuja kutajwa na kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza ombi lolote kwakuwa kesi hiyo haitasikilizwa mahakamani hapo.

Kaganda alidai kuwa kesi hiyo bado ipo katika hatua ya upelelezi ambao bado haujakamilika na kwamba miongozi mwa vitu wanavyovichunguza ni pamoja na umri wa mshtakiwa huyo.

Aliongeza kuwa katika cheti cha kuzaliwa kilichooneshwa mahakamani hapo na Fungamtama, alidai kuwa hawawezi kukiamini kwani kina jina la Dayana Elizabert wakati mshtakiwa anaitwa Elizabert Michael.

"Mheshimiwa hakimu tunaomba tupewe hicho cheti tukichunguze pia tupewe muda tuchunguze zaidi kuhusu umri wake,kama itabainika ana miaka chini ya 18 mshtakiwa ana haki zote za kushtakiwa katika mahakama ya watoto"alisema Kaganda.

Akitoa uwamuzi wa maombi hayo hakimu Mmbando aliutaka upande wa utetezi kusubiri kesi hiyo itakapowasilishwa katika Mahakama Kuu ndipo wawasilishe maombi hayo kwakuwa mahakama hiyo hivi sasa haina mamlaka.

"Mahakama hii inajua kuwa shauri lililo mbele yake ni la mauaji,hatuna mamlaka ya kutoa uamuzi wowote kwa sasa ,maombi yoyote yafanyike Mahakama Kuu"alisema Mmbando.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 21, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.Katika kesi hiyo Lulu anashtakiwa kwa kudaiwa kusababisha kifo cha msanii mwenzake wa filamu, Steven Kanumba.






No comments:

Post a Comment