14 March 2012

Yanga yazua jipya TFF

*Yataka mechi dhidi ya Azam ifutwe
*Kuivaa Lyon leo, Simba na Polisi Dom


Baadhi ya wachezaji wa Yanga na viongozi wao wakishangilia moja ya bao lililopatikana katika moja ya mechi za Ligi Kuu. Baadhi ya wachezaji hao wamefungiwa kutokana na kuhusika katika vurugu zilizotokea wiki iliyopita kati ya mechi yao na Azam FC iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. (Picha ya Maktaba)

Na Zahoro Mlanzi
KLABU ya Yanga, imeitaka Kamati ya Ligi Kuu Bara iliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kufuta kadi saba za njano na mbili nyekundu walizopewa wachezaji wao wakati wa mechi dhidi ya Azam FC na pia kufuta matokeo ya mechi hiyo.

Mbali na hilo, Yanga pia imepinga maamuzi yaliyotolewa na mwamuzi Islael Nkongo wakidai aliipendelea Azam katika mechi ambayo Yanga ililala kwa mabao 3-1.

Pamoja na madai hayo ya Yanga, Kamati hiyo ilikutana juzi na kujadili mechi mbalimbali za ligi hiyo ikiwemo ya Yanga na kuwapa adhabu wachezaji watano huku ikimpongeza Nkongo kwa jinsi alivyokuwa makini katika mechi hiyo.

Akijibu swali kuhusu taarifa za Yanga kukata rufaa kwa kamati hiyo kutokana na kutoridhishwa na uamuzi wa Nkongo, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura alisema ni kweli Yanga imekata rufaa na barua yao imewafikia tangu juzi.

"Kweli Yanga imeleta barua ya rufaa na tayari imeshakabidhiwa kwa kamishna wa mechi hiyo ambaye ataipeleka kwa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ili kujadiliwa," alisema Wambura.

Alisema pia walidai kwamba makosa ambayo walifanya wachezaji wao na kupewa kadi hizo ni sawa na yale waliyofanya wachezaji wa Azam lakini cha kushangaza Azam hawakupewa kadi zozote.

Alisema katika barua hiyo, Yanga inadai kadi zote walizooneshwa wachezaji wake katika mechi hiyo zifutwe pamoja na matokeo ya mechi hiyo kwani uamuzi uliokuwa ukitolewa na Nkongo hawakubaliani nao.

Kabla ya kujibu swali hilo, Wambura alizungumzia kuhusu kikao cha juzi cha kamati hiyo ambacho kilitoa maamuzi mbalimbali kuhusu mechi za ligi kuu na Ligi Daraja la Kwanza.

Alisema Villa Squad imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya washabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi dhidi ya Azam iliyochezwa Februari 15, mwaka huu Uwanja wa Chamazi, Dar es Saalam.

Pia klabu hiyo imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa uwanjani kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa Februari 19, mwaka huu Uwanja wa Manungu. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 8(13) ya ligi hiyo.

"Nayo Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na washabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi dhidi ya Azam iliyochezwa Machi 10, mwaka huu. Pia klabu hiyo imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa mujibu wa Kanuni ya 25(d) baada ya kuoneshwa kadi kuanzia tano kwenye mechi moja," alisema Wambura.

Alisema Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Yanga, amefungiwa mechi sita za ligi kuu na kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya kuoneshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumshambulia mwamuzi Nkongo.

Wengine wa Yanga waliopewa adhabu ni kutokana na mechi hiyo ni Nurdin Bakari na Omega Seme, wamefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000 kila mmoja, Jeryson Tegete amefungiwa miezi sita na faini ya sh. 500,000 na Stephano Mwasika amefungiwa mwaka mmoja na faini ya sh. milioni moja kwa kumpiga mwamuzi Nkongo.

Aliongeza kwamba, pia mchezaji Juma Mohamed wa Polisi Dodoma amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya kuwashambulia watazamaji kwa chupa ya maji katika mechi kati ya timu yake na Villa Squad.

Katika hatua nyingine, Yanga leo itashuka uwanjani kuumana na African Lyon katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Simba watakuwa wageni wa Polisi Dodoma katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Jamhuni, Dodoma.







No comments:

Post a Comment