Na Godfrey Ismaely, Dar es Salaam
UMOJA wa Ulaya (EU) umehaidi kuiwezesha Tanzania kwa hali na mali hususan kuijengea uwezo wa kupata huduma ya maji safi na salama katika maeneo mbalimbali ili Watanzania waweze kunufaika.
Wazo la kuijengea Serikali uwezo katika mpango wezeshi wa hupatikanaji wa maji safi na salama ni fursa moja wapo ambayo inaelezwa na wachambuzi wa masuala ya kijamii kuwa, itawanufaisha Watanzania wengi kutokana na maji hupatikanaji wake kuwa changamoto kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa ubalozi huo kupitia hotuba yake ambayo ilitumwa kwa vyombo vya habari juzi kutoka kwa Balozi wa EU Tanzania, Bw.Filiberto Sebregondi mara baada ya kutiliana sahihi na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Servacius Likwelile jijini Dar es Salaam alisema, dhamira ya umoja huo ni kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana nchini kwa wakati.
"Umoja wa Ulaya ni rafiki wa muda mrefu na Tanzania, hivyo mahusiano yetu yamejikita katika kuijengea uwezo katika nyanja zote ikiwemo demokrasia imara, wakati wote wa shida na hata majanga yanapojitokea ikiwemo shughuli za maendeleo,"
Alisema, mbali na hayo pia umoja huo upo karibu na Tanzania ili kuhakikisha kwamba changamoto mbalimbali ambazo zinaikabili Dunia kwa sasa yakiwemo mabadiliko ya hali ya hewa, mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi na vitendo vingine havijitokezi hapa nchini.
"Ndiyo maana siku ya leo (juzi) tuna kila sababu na furaha ya pekee kuyatimiza haya. Ni wazi kwamba tupo hapa kwa jambo moja la msingi tena la muhimu kwa maendeleo ya Tanzania, ambapo tunaigia makubaliano sisi (Umoja wa Ulaya) kutiliana sahihi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kusaidia mpango wa maendeleo wa milenia hasa kuwajengea uwezo hupatikanaji wa huduma ya maji safi na salama," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo ambayo ilimnukuu Balozi huyo.
Pia taarifa hiyo ilifafanua kuwa Umoja wa Ulaya unaamini kuwa uimarishaji wa huduma bora hasa maji safi na salama kwa wananchi ndiyo njia pekee ya kuyafikia malengo ya kuwajengea uwezo katika afya zao.
"Maji kwa sasa ndiyo kipaumbele chetu kikubwa katika jamii ikiwemo Serikali ya Tanzania ambayo ni miongoni mwa nchi zaidi ya 35 zilizofanikiwa kuandaa mchanganuo mzuri, ambao umewezesha ipatiwe kiasi cha euro milioni 51.51 (zaidi ya bilioni 108 za kitanzania).
"Fedha ambazo zitasaidia uboreshaji wa miundombinu ya maji safi na salama ambayo yanaweza kutumiwa na Watanzania zaidi ya 500,000 kwenye makazi yapatayo 140,000 katika miji ya Lindi, Sumbawanga na Kigoma," iliongeza sehemu ya taarifa hiyo.
Alisema, EU inaamini kuwa changamoto ambayo Tanzania inayo kwa sasa ni kuhakikisha hutoaji wa huduma ya maji safi na salama inapatikana kila kaya ili kulinda afya za Watanzania.
"Amna afya kama huduma ya maji haipatikani tena katika hali ya usafi... mabibi na mabwana niwahakikishieni kwamba Umoja wa Ulaya umejitolea kwa Watanzania ili kuhakikisha kwamba huduma ya maji safi inapatikana na kila mmoja anahifurahia," ilifafanua taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment