*Aonya mgomo waliofanya uwe wa mwisho
*Aeleza jinsi walivyoienyesha Serikali
*Awapiga kijembe wanaharakati nchini
Peter Mwenda na Rachel Balama
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, ameahidi kuyafanyia kazi madai yote ya madaktari yaliyo ndani ya uwezo wa serikali na kuonya kuwa mgomo huo uwe wa mwisho.
Rais alitoa kauli jana wakati akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam katika ukumbi wa Daimond Jubilee kuhusu sakata la mgomo wa madaktari.
"Serikali ipo tayari kutekeleza madai yote ya madaktari yaliyopo ndani ya uwezo wake na nisiwadanganye tuwatekelezea yaliyo nje ya uwezo wetu, japo tutajitaidi," alisema Rais Kikwete.
Alisema madai hayo yatapatiwa ufumbuzi kwa kuwa sekta ya afya inatakiwa kupewa kipaumbele kuliko sekta nyingine. "Ninaheshimu ahadi zinazotolewa na serikali na ninawahakikishia madaktari madai yao tutayashughulikia na yatakwisha tu," alisisitiza Rais Kikwete.
Aliwataka madaktari hao kumuamini na kuwa wakifanya hivyo mambo yao yatashughulikiwa na yatakuwa mazuri. Rais Kikwete alisema mgomo wa madaktari unagusa maisha ya watu, tofauti na ule wa daladala, hivyo uwe wa mwisho.
Aliwataka madaktari hao kutimiza wajibu wao kisheria ambao unawataka wafanyakazi wa sekta ya afya, umeme na maji wasigome. "Daladala zikigoma watu watatembea kwa miguu watafika, lakini daktari akigoma mtu akafa hakuna njia ya kurejesha uhai wake," alisema Rais Kikwete.
Kuhusu shinikizo la madaktari la kutaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hadji Mponda na Naibu wake, Dkt. Lucy Nkya, alisema; "Hilo si tatizo, lakini hao wakitolewa atakuja mwingine na hali inaweza kuwa vile vile, kinachotakiwa ni kutengeneza mfumo utakaopatia ufumbuzi madai yenu na si mawaziri kujiuzulu au mimi kuwaondoa."
Alisema mawaziri wanaweza kubadilishwa na kutolea mfano kama ambavyo amekuwa akifanya kwa Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli.
Alisema kuwa kutokana na sekta hiyo kupewa kipaumbele serikali imekuwa ikichukua hatua kadhaa kukabiliana na changamoto hizo, ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti kuanzia mwaka 2005 kutoka sh. bilioni 271.2 hadi kufikia trilioni 1.2 kwa mwaka huu.
Alisema bajeti hiyo imeongezeka mara sita na sekta hiyo imepandishwa kutoka nafasi ya sita hadi nafasi ya tatu.
Alisema yapo mambo mema ambayo serikali imeyafanya kwa kuongeza mishahara ya madaktari na wauguzi kwa asilimia 100 mwaka 2006.
Kuhusu madai ya madaktari hao kuwa mahusiano yao na wizara si mazuri, alisema atajitaidi kuhakikisha yanakuwa mazuri. Alisema hilo ni jambo la kawaida, kwani hata mawizarani inatokea waziri anakuwa haelewani na naibu waziri, au katibu mkuu na waziri.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete aliwashangaa wanaharakati wa kutetea haki za binadamu kwa kushabikia mgomo huo badala ya kutetea uhai wa watu.
"Uhai wa binadamu ni kitu muhimu sana kuliko kitu chochote, sasa hawa wanatetea haki gan? Badala ya kutetea madaktari wasitishe mgomo ili watu waishi wao wanashabikia," alisema na kuongeza;
"Nimefadhaishwa sana na watu wanaojiita wanaharakati, kwani hata kama ni agenda ni za kisiasa lakini si hivyo, wasitafute umaarufu kwa njia hiyo," alisema.
Awali Rais Kikwete alieleza jinsi madaktari hao walivyoienyesha serikali yake tangu mwanzo wa mgomo hadi kufikia hatua ya sasa, ambapo wamekubali kurejea kazini.
No comments:
Post a Comment