15 March 2012

Watumishi afya wahimizwa kuboresha huduma nchini

Na Mwandishi Wetu, Mwanza
WATUMISHI wa sekta afya wameshauriwa kutoa huduma bora ya uzazi ili kupunguza vifo vya wajawazito vinavyosababishwa na watu kufuata  tiba kwa waganga wa jadi.

Ushauri huo ulitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Bw. Philemon Shelutete, alipokuwa akifungua semina ya utambulisho wa kampeni ya mama mjamzito kwa madiwani na wenyeviti wa mitaa wilayani Geita.

Bw. Shelutete alisema kuwa huduma bora za wahudumu wa afya kwa wajawazito inaweza kuwa moja ya ngao zinazoweza kuzuia ongezeko la vifo vya wajawazito nchini.

Aliitaka jamii ya Watanzania kufahamu umuhimu wa mjamzito kupata huduma za hospitalini badala ya kuwashauri kwenda kwa waganga wa jadi, kwani kufanya hivyo ni kuhatarisha maisha ya mama na mtoto aliye tumboni.

“Badala ya kuwaelekeza wajawazito kwenda kuonana na matabibu walioko katika vituo vyetu vya afya ili wapate ushauri wa kitaalamu, tunawapeleka kwa waganga wa kienyeji…kwenye nyumba za msonge,” alisema Bw. Shelutete.

Aliongeza kuwa; “Jambo hili ni hatari kwa saba sababu yawezekana mtoto amekaa vibaya tumboni, au hana damu ya kutosha.”

Alisisitiza umuhimu wa kuwahimiza wajawazito waende kwenye vituo rasmi vya afya badala ya kwenda kwa waganga. Semina hiyo ni mwendelezo wa kampeni ya afya ya uzazi inayoendeshwa na Shirika la Tandabui Health Access Tanzania (THAT)/Afya Redio katika wilaya za Nyamagana, Ilemela na Geita zote za mkoani mwanza.

Akizindua  kampeni hii wiki iliyopita Mjini Mwanza,  Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Bw. Said Malinzi, alisema hali vifo vya wajawazito bado ni mbaya mkoani Mwanza na kushauri asasi nyingine zisizo za kiserikali kuiga mfano wa  THAT/Afya Redio kwa kutoa semina za mara kwa mara kwa watumishi wa idara ya afya ili kuwawezesha kutoa huduma bora.

Akitambulisha mradi huo,  Mratibu wa Mradi wa Afya ya Mama na Mtoto, Bi Jane Benedict, aliyataja malengo ya mradi huo kuwa ni pamoja na kutambua chanzo cha vifo vya vinavyotokana na matatizo ya uzazi na kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya kadi ya kliniki kwa wajawazito na jamii kwa ujumla.


No comments:

Post a Comment