Na Zourha Malisa
MAMLAKA ya Hali ya Hewa (TMA) imewataka wakazi wa mabondeni kuhama ili kunusuru maisha yao na mali zao kutokana na kuwepo tishio la mabadiliko ya hali ya hewa nchini yanayoweza kusababisha mvua kubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Dkt.Emmanuel Mpeta, alisema hali hiyo inachangiwa na ongezeko dogo la joto linalotarajiwa katika ukanda wa Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi.
Alisema hali hiyo inatarajia kuongezeka hivyo kusababisha kupungua au kuongezeka kwa mvua katika baadhi ya katika baadhi ya maeneo.
Bw. Mpeta alisema kuna misimu ya mvua za mvuli na masika, hivyo wataalamu wa mamlaka hiyo kwa kuzingatia joto la bahari ya Hindi imeonekana kutakuwa na mabadiliko kidogo ukanda wa kaskazini mashariki na pwani ya kaskazini kanda ya ziwa.
"Sehemu zinazopata mvua mara mbili kwa mwaka zitakuwa na mvua ya wastani, lakini kuchukua tahadhari ni lazima kwani matukio ya mvua kubwa hayazuiriki," alisema.
Alisema kuwa kutakuwa na mvua ya wastani zitakazotosheleza upatikanaji wa chakula nchini ingawa mabadiliko yoyote yanaweza kutokea.
Bw. Mpeta alisema taasisi za maafa na wadau husika wanashauriwa kuchukua hatua muafaka za maandalizi ya kukabiliana na majanga ya hali ya hewa yanayoweza kutokea.
No comments:
Post a Comment