*Shahidi adai alihusika 'kuchakachua' matokeo
Na Rehema Mohamed
ALIYEKUWA Meneja Kampeni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi Mkuu mwaka 2010, Kanali mstaafu, Abdulrahiman Kinana, amehusishwa katika uchakachuaji wa kura za ubunge wa Jimbo la Segerea zilizompa ushindi Dkt. Makongoro Mahanga.
Hayo yameelezwa jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakati shahidi wa sita katika kesi ya kupinga matokeo ya ubunge wa jimbo hilo Bw. Livingstone Rugema (31), akitoa ushahidi wake mbele ya Jaji Profesa Ibrahim Juma.
Bw. Rugema alimtaja Bw. Kinana akidai kuwa, alifika katika ukumbi wa Anatoglou ambao ulitumika kufanya majumuisho ya kura za ubunge kisha kuondoka na msimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo Bw. Gabriel Fuime, kama matokeo hayajatangazwa.
Alidai Bw. Kinana na Bw. Fuime walipanda gari moja na kwenda kusikojulikana wakiwa peke yao bila polisi au wakala wa chama kingine tofauti na CCM.
Aliongeza kuwa, kuondoka kwao kuliwapa wasiwasi watu wengi waliokuwa ukumbini hapo hivyo matokeo yaliyotangazwa hayakuwa halali.
“Mkurugenzi Bw. Fuime kuondoka na mtu wa itikadi ya CCM bila polisi wala mawakala wa vyama vingine, ilitupa wasiwasi kwani huenda matokeo yaliyotangazwa hayakuwa halali,” alisema.
Alilisema kutokuwa na imani na matokeo hayo pia kunachangiwa na matukio yaliyojitokeza muda mfupi baada ya Bw. Kinana na Bw. Fuime kuondoka.
“Kuna tukio la mtu kukamatwa na mihuri pamoja na mfuko wa fomu za kufanyia majumuisho ya kura za mbunge, mtu huyu baada ya kuhojiwa alisema mfuko huo ulikuwa na chipsi,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Bw. Rugema alidai Mwanasheria wa Manispaa ya Ilala aliingia katika majumuisho ya kura Kata ya Segerea jambo ambalo liliwapa wasiwasi.
Alidai Mwanasheria huyo hakupaswa kuingia kwa mujibu wa sheria za uchaguzi na baada ya kuhoji uwepo wake kwa msimamizi wa uchaguzi wa kata hiyo, alidakia mahojiano na kusema mtu mwenye wasiwasi naye akafungue kesi mahakamani.
“Katika vituo vya majumuisho ya kura, kawaida huwa anaingia mgombea mwenyewe, wakala wake au msimamizi wa uchaguzi wa kata kama kuna mtu mwingine tofauti tunatakiwa tujulishwe lakini kwa huyu Mwanasheria hakutambulishwa kwetu,” alidai.
Aliongeza kuwa, pamoja na majibu hayo hapakuwa na suluhisho kuhusu suala hilo kutoka kwa msimamizi wa kituo na kusisitiza kuwa, majumuisho ya kura ngazi ya kata yalileta utata na kufanya warudie kuhesabu mara tatu ambapo mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alipata kura 5,496 na mgombea wa CCM alipata kura 3,664.
No comments:
Post a Comment