Na Eliasa Ally, Iringa
NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Bi. Ummy Mwalimu amesema watu wanaoendelea kuibeza Serikali kuwa kuanzisha shule za sekondari katika kata haijafanya kitu upeo wao ni mdogo pia mtazamo kuhusiana na maendeleo bado upo chini hivyo wanapaswa kubadilika mapema.
Alisema shule hizo ni sawa na mwanga mpya kwa jamii hatua ambayo alifafanua kuwa ni kama mshumaa ambao umewashwa gizani na unamulika mbali zaidi.
Akizungumza jana mkoani Iringa wakati wa uzinduzi wa kongamano la pili la wanawake na viongozi wa Mkoa wa Iringa alisema, Serikali ina kila kitu cha kujivunia kwa kuzijenga sekondari za kata ambazo kwa sasa zinawapokea maelfu ya vijana ambao awali walikuwa wanakosa shule.
Alisema, kwake binafsi anaunga mkono juhudi za serikali za kuanzisha shule za sekondari za kata kwa kuwa zimetoa mwanga mkubwa kwa jamii hususan waliokuwa wanakosa elimu kutokana na uchache wa shule.
"Ninasikitishwa sana na watu ambao wanabeza kila kitu ambacho kinafanywa na Serikali hasa kuanzishwa kwa shule za sekondari za kata, kwa kweli nia ya Serikali ni njema na shule hizo ni msaada mkubwa sana kwa watoto wetu wa vijijini baada ya kuhitimu darasa la saba, kinachotakiwa hapa wananchi watoe maoni na washirikiane na serikali ili kuboresha penye matatizo, shule hizi ziwe sawa na zile za siku nyingi," alisema Bi.Mwalimu.
Aidha, aliongeza kuwa wananchi wasipinge kila kitu ambacho Serikali imefanya kwa kuwa kuna kila sababu ya kupongeza mengine ambayo yanaonekana ni mazuri na yale ambayo yanaonekana kiwango chake hakiridhishi anaamini wakitoa mawazo yao yatakuwa mazuri kuliko kuishutumu Serikali.
"Serikali kwa kuungana na wananchi imeanzisha shule za sekondari za kata, na kupeleka walimu wachache, kwa muda sasa kwa pamoja, sisi na serikali yetu kinachotakiwa ni kutambua changamoto ambazo zinazikabili shule hizo za kata na tupange nini cha kufanya ili shule hizo ziwe sawa na zingine," aliongeza.
No comments:
Post a Comment