Na Moses Mabula, Tabora
WANANCHI wa Jimbo la Kaliua mkoani Tabora wamesema katika mabidiliko ya Katiba Mpya ambayo mchakato wake unaendelea hapa nchini wadhifa wa Rais ufutwe na ibakie nafasi ya Waziri Mkuu kwa kuwa ndiye anayewajibika katika shughuli mbalimbali za serikalini.
Mapendekezo hayo waliyatoa katika mdahalo wa uwazi na uwajibikaji kwa viongozi wa ngazi ya kata na mitaa uliondaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Tabora NGos Cluster chini ya ufadhili wa The Foundation for Civil Society kutoka jijini Dar es salaam.
Akichangia maoni yake katika mdahalo huo, Bi.Asha Shabani alisema, ili kuwepo na uwajibikaji kwa viongozi wa ngazi zote serikalini ni lazima izingatiwe wakati wa kuunda Katiba Mpya kuwe na mfumo wa utawala kama Uingereza ambapo Waziri Mkuu ndiye atakuwa mwenye mamlaka yote serikalini.
Alisema, kwamba mfumo uliopo sasa Rais yupo zaidi kisiasa hivyo hali hiyo inachangia kushindwa kuwachukulia hatua wasaidizi wake ambao wanatuhumiwa kufanya vibaya katika utendaji kazi wao kwa wananchi.
Kuhusu uajibikaji kwa viongozi ngazi ya kata na mitaa, Bi. Shabani alisema viongozi hao wanapaswa kujenga utamaduni wa kusoma taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi wao ili kuondoa migongano ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara na kusababisha mitafaruku mikubwa ambayo alidai si ya lazima katika jamii.
Pia alisema, wananchi wenzake wanapaswa kujenga utamaduni wa kuhudhuria katika mikutano ya hadhara na kwamba iwapo watakuwa na utamaduni huo wataweza kufahamu mipango ya maendeleo katika maeneo yao pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo badala ya kubakia kuitupia lawama serikali pekee.
Alisema, imejengeka tabia kwa wananchi kuilaumu Serikali kwamba haiwatendei haki wananchi wake, kwa madai haiwashirikishi katika mikutano ya hadhara na kujisahau kuwa ndio wana wajibu mkubwa kufahamu nini Serikali yao inatarajia kupanga kuhusu kazi za maendeleo
“Tumekuwa wepesi wa kuilaumu Serikali mara hivi...tujenge utamaduni wa kuhudhuria mikutano mikuu ya vijiji pamoja na ile ya Baraza la Madiwani, hapo mkihudhuria vikao hivyo mtaweza kufahamu nini serikali yenu imepanga kuhusu maendeleo yenu," aliongeza.
Aidha, alieleza kuwa iwapo wananchi watahudhuria kikamilifu katika mkutano mkuu wa kijiji watapata fursa ya kuweza kujadili kero na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao na hatimaye kuzipatia ufumbuzi.
Awali Mratibu wa shirika hilo, Bw. Cathibety Ndogoma alisema, lengo kuu la mdahalo huo ni kuhamsha ufahamu kwa wananchi ili waweze kuelewa wajibu wao na wajibu wa viongozi serikalini.
No comments:
Post a Comment