15 March 2012

Business Times yaanza kwa kishindo NSSF

 Meneja wa timu ya soka za Kampuni ya Business Times, 'The Bize', Masoud Sanani akiwapa mawaidha baadhi ya wachezaji wa timu hiyo, wakati wa mapumziko kwenye mchezo wao dhidi ya TSN wa michuano ya NSSF Cup uliopigwa juzi katika viwanja vya TCC Chang'ombe, The Bize walishinda kwa mabao 6-1. (Picha na Victor Mkumbo)

Na Victor Mkumbo
TIMU za Kampuni ya Business Times (BTL), 'The Bize FC' na The Bize Queens, juzi zilianza vyema katika mechi zake za kwanza za mashindano ya vyombo vya habari yanayoandaliwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) yanayofanyika kwenye viwanja vya Sigara na DUCE, Dar es Salaam.

Katika soka The Bize FC iliikung'uta TSN mabao 6-1, huku dada zao wakiichanganya Changamoto kwa kuipa kipigo cha mabao 25-2.

The Bize FC ilianza mechi hiyo kwa nguvu na kupeleka mashambulizi kama nyuki kwa wapinzani wao, ambapo dakika ya saba kupitia kwa Jemedari Said ambaye alipokea pande safi kutoka kwa Zahoro Mlanzi.

Dakika ya 16 George Denis aliipatia timu hiyo bao la pili, baada ya kuwatoka mabeki na kuachia shuti kali lililojaa wavuni moja kwa moja.

Wakitandaza kandanda safi, The Bize walipata bao la tatu dakika ya 20 mfungaji akiwa Omari Dogorino ambaye alipokea pasi ya Mlanzi, huku bao la nne liliwekwa kimiani na Ally Kilo kwa shuti kali la mbali.

Kipindi cha pili The Bize, iliandika bao tano dakika 55 lililopachikwa na Denis kwa shuti kali baada mabeki kujichanganya.

Dakika ya 85 mwamuzi wa mchezo huo, alimzawadia kadi nyekundu beki wa TSN, Carlos Mlinda baada ya kumkwatua kiungo mahiri wa The Bize, Mlanzi ambaye alikuwa anakwenda kufunga bao.

The Bize iliandika bao la sita dakika ya 87 kupitia kwa Ibrahim Kajala, baada ya kuwatoka mabeki na kumpiga chenga kipa wa TSN na kuukwamisha mpira wavuni.

TSN walipata bao la kufutia machozi dakika ya 88 kupitia kwa Abubakari Kombo kwa shuti kali la mbali kutoka katikati ya uwanja na kujaa wavuni baada ya kipa wa The Bize, Eckland Mwaffisi kutoka golini.

Katika mchezo wa netiboli, The Bize Queens waliweza kuichachafya Changamoto kwa mabao 27-2, ambapo mpaka mapumziko washindi hao walikuwa mbele kwa mabao 14-0.

Kipindi cha pili The Bize Queens waliweza kutumia vyema udhaifu wa wapinzani wao na kupachika mabao ambapo wafungaji wake Rehema Mohamed, pamoja na Saluketa Mhina walimudu vyema kupachika mabao.




No comments:

Post a Comment