Na Mwandishi Maalum, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amekutana na uongozi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) na kueleza kuna haja kwa vyombo vya habari na watendaji wake nchini kufuata maadili ya fani hiyo kwani maadili ndio nguzo kuu katika utendaji kazi.
Dkt.Shein aliyasema hayojana wakati alipokuwa na mazungumzo na uongozi wa MCT, ulioongozwa na Makamu Mwenyekiti wake, Bw.Chande Omar ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, uliofika Ikulu mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo Rais aliueleza uongozi huo kuwa migogoro mingi inayotokea katika vyombo vya habari inatokana na kutofuatwa maadili ya sekta hiyo.
"Hivyo kuna haja ya kulisimamia kwa nguvu zote jambo hilo, kwani litaijengea heshima baraza, bodi pamoja na viongozi wake," alisema.
Alisema, kwa upande wake amevutiwa na malengo na mikakati ya MCT tangu kuanza kazi zake, hatua ambayo imepelekea kupatikana mafanikio makubwa katika sekta ya habari hapa nchini.
Dkt. Shein alisema, licha ya kuwa baraza hilo lina kazi nyingi na ngumu lakini ipo haja ya kulisiamamia suala la maadili ili liweze kuiweka sekta ya habari katika hatua nzuri ikiwemo kuzingatia uwazi zaidi.
Aliueleza uongozi huo kuwa, kwa kawaida jamii inatakiwa kupata habari zilizo sahihi ili kuepusha migogoro katika jamii, hivyo MCT wana kazi ngumu ya kuhakikisha jamii inapata habari sahihi na vyombo vya habari pamoja na taasisi za habari zinafuata maadili.
Dkt.Shein alisema, jambo la kuzuia migogoro isitokee juu ya vyombo vya habari ni kusisitiza kufuatwa kwa maadili na kulitaka baraza kupanga taratibu zake vizuri katika kuhakikisha kila baada ya muda linavikumbusha vyombo vya habari maadili ya fani hiyo.
"Mimi nimekuja na mfumo wa kutoa habari kwani wananchi wanahitaji kupata habari juu ya nchi yao na maendeleo yao...hakuna haja ya kuficha habari," alisema Dkt. Shein.
Dkt.Shein alisisitiza juu ya suala zima la kuwepo kwa kumbukumbu na historia katika vyombo vya habari nchini kwani Zanzibar ina historia kubwa katika sekta hiyo kwa Afrika Mashariki na Afrika nzima kwa jumla.
Pia alilipongeza baraza hilo kwa namna linavyotoa mafunzo yake kwa vyombo vya habari pamoja na namna linavyosimamia suala zima la upatanishi.
Naye Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Bw. Kajubi Mukajanga alieleza kuwa baraza lilianzishwa mwaka 1995 na liliundwa kutokana na haja ya kuwepo kwa usimamizi wa vyombo vya habari nchini Tanzania baada ya kufunguliwa milango kwa vyombo vya habari binafsi nchini.
Alisema, kutokana na hali hiyo ndipo mwaka 1997 kazi rasmi ilianza na mwaka 2003 likafungua ofisi zake mjini Zanzibar ambapo kwa sasa baraza hilo lina wanachama 15 visiwani humo vikiwemo vilabu vya waandishi wa habari na taasisi nyingine.
Kwa upande wa baraza hilo, Katibu huyo alieleza kuwa limekuwa likitoa mafunzo kwa vyombo vya habari na watendaji wake Unguja na Pemba, kufanya upatanishi na kusimamia demokrasia, kuiendeleza siku ya vyombo vya habari duniani kila ifikapoMei 3, kutoa machapisho sanjari na kufanya utafiti.
Naye Meneja wa Udhibiti wa Viwango wa Baraza hilo, Bi.Pili Mtambalike alisema uongozi huo unalifanyia kazi suala zima la maadili kwa vyombo vya habari huku akieleza matumaini yao makubwa juu ya mabadiliko ya sheria.
No comments:
Post a Comment