13 March 2012

Viwanda vinavyotumia kuni vyashauriwa

Na Florah Temba, Kilimanjaro
MKURUGENZI wa Misitu na Nyuki nchini Dkt. Felician Kilahama amesema amesikitishwa na vitendo vya ukataji wa miti ya asili katika misitu na  kwenye vyanzo vya maji, kwa matumizi ya kuni katika baadhi ya viwanda ambavyo vinatumia nishati hiyo kuendeshea shughuli zake.

Alisema hali hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira hivyo ni vyema wahusika wakasitisha shughuli hiyo mara moja.

Dkt. Kilahama aliyasema hayo mwishoni mwa wiki mara baada ya kutembelea Kiwanda cha Kutengeneza Karatasi cha China kilichopo mjini Moshi Mkoa wa Kilimanjaro na kukuta rundo la magogo yanayotokana na miti ya asili.

Miti ambayo alisema, huwa inapandwa katika vyanzo vya maji ambapo alielezwa kuwa kuni hizo hupelekwa kiwandani hapo na wadau mbalimbali kupitia vibali maalumu kutoka kwa maofisa misitu na maliasili.

Pamoja na Mkurugenzi huyo kukuta magogo hayo ambayo yanaonekana kuvunwa katika misitu na maeneo mengine kinyume cha taratibu uongozi wa kiwanda hicho ulimueleza kuwa wenyewe haujui kama kuna miti ambayo hairuhusiwi kukatwa na wala hawaelewi sehemu magogo hayo yamevunwa.

Dkt. Kilahama alisema, ni makosa makubwa wataalamu kutofika katika viwanda kama hivyo ambavyo vinatumia nishati ya kuni kwa ajili ya kuendeshea shughuli zake kutokana na kwamba viwanda vingi ambavyo hutumia nishati hiyo huvuna na kusafirisha magogo kinyume cha sheria.

Alisema, kimsingi viwanda ambavyo vinategemea nishati ya kuni kwa ajili ya kuendeshea shughuli zake vinahitajika kuwa na chanzo cha upatikanaji wa kuni hizo yaani shamba la miti ili kuepuka uharibifu wa misitu na ukataji wa miti ovyo.

“Ni makosa makubwa wataalamu wetu wa misitu kutofika hapa kuwatembelea, lakini sasa tunataka kuni ambazo mnatumia zitoke kwenye mpango ambao ni endelevu na si kuharibu mazingira, pia mnaweza kutafuta njia nyingine ya kutumia tofauti na kuni,”alisema Dkt. Kilahama.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo aliwataka maofisa misitu na maliasili kubadilika na kuepuka kutumiwa vibaya na wafanyabiashara kwa maslahi binafsi na kuisaliti taaluma yao.

Alisema, ni vema viongozi hao wakaacha kushirikiana na wafanyabiashara kuhujumu mazingira ikiwa ni pamoja na kuogopa zawadi ambazo huwa wanapewa.

“Msishirikiane na wafanyabiashara wabovu, epukeni vishawishi na vizawadi vya wafanyabiashara, kwani ni bora mtu ukafa maskini kuliko ukaisaliti taaluma yako kwa kushirikiana na wafanyabiashara,”alisema.

Kwa upande wake, Bw. Emanuel Massenga mmoja wa viongozi katika kiwanda hicho alisema, kiwanda hicho kilianza kufanya kazi mwaka 2008 na kwamba kwa siku wanatumia mita za ujazo tani tatu hadi tano za kuni ambapo huwa wanazipata kutoka kwa wadau mbalimbali wengi wao wanatokea katika Wilaya ya Hai mkoani humo.

Bw.Massenga alisema, ni vema  wakawa wanatembelewa mara kwa mara na viongozi wa misitu na maliasili ili kupewa elimu na maelekezo ikiwa ni pamoja na kuambiwa aina ya miti ambayo haitakiwi kukatwa ili wanapopelekewa kuni wazikatae.

“Sisi hapa kiwandani hatujui chochote na kama kuna maelekezo tunapaswa kupewa, kwani hata aina ya miti hatuijui tunaomba ushirikiano kutoka kwenye ofisi yako ili kufanikisha hili,”alisema Bw. Massenga.

No comments:

Post a Comment