Na Mwandishi wetu
UWAJIBIKAJI ni sifa mojawapo ya kuwa kiongozi bora kwa kuhakikisha utawala unaowajibika ili uweze kuchangia katika utoaji huduma zitakazowawezesha wananchi kuboresha maisha na kutokomeza umaskini katika jamii zao.
Bila utawala bora unaosimamia haki, usawa, uwazi na uwajibikaji malengo mbalimbali katika Mkakati huu wa Kuinuia Uchumi na kupunguza umaskini yanaweza yasifikiwe.
Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania, (MKURABITA). Ni Mpango ulioanzishwa na Serikali kwa lengo la kumilikisha uchumi kwa watanzania ili kuwawezesha kutumia mtaji uliofichika katika rasilimali na biashara zao waweze kushiriki katika mchakato wa uchumi rasmi unaotawaliwa na sheria.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba, wananachi wengi wanamiliki rasilimali na kuendesha ambazo hazina uhai wa kisheria katika sekta isiyo rasmi.
Mtaji uliofichika katika rasilimali na biashara hizo hautambuliki. Hivyo wamiliki wake hawajumuiki kikamilifu katika uchumi rasmi.
Hivyo hawanufaiki na fursa zilizopo pia hawachangii kikamilifu katika kukuza uchumi wa nchi.
Kwa hiyo urasimishaji wa rasilimali na biashara unakusudiwa kuzipa rasilimali na biashara za walio wengi uhai wa kisheria
Viongozi wengi wamekuwa na tabia ya kuwatumikia wananchi yanapotokea matatizo na kujenga taswira mbaya kwa jamii.
Mkuu wa MKURABITA, Injinia Ladislaus Salema amesaidia kufanya kazi iliyorahisisha kwa kiasi kikubwa wajibu wa Kamati ya Uongozi kuleta maendeleo.
Spika wa Bunge la Tanzania, Bi. Anne Makinda ameyasema hayo katika hafla ya kumuaga Bw.Salena hivi karibuni baada ya kustaafu kuwa, “Mtakumbuka katika awamu ya kwanza yaani ile ya kufanya tathmini ya sekta isiyo rasmi, serikali iliitumia Taasisi ya Uhuru na Demokrasia inayoongozwa na Mtaalamu maarufu wa Uchumi, Dk. Hernando de Soto wa Peru kama Mshauri Mwelekezi.”
Anasema, serikali iliridhia ripoti na kuruhusu kuanza kwa awamu ya pili kulikolenga kuandaa maboresho yaliyozingatia mapungufu yaliyoonekana katika awamu ya kwanza.
Makubaliano ya awali yalikuwa ni kwa mshauri mwelekezi kuendelea kusimamia maandalizi ya maboresho.
“Lakini Mratibu Salema aliishauri Kamati ya Uongozi juu ya umuhimu wa shughuli ile kufanywa na Watanzania wenyewe na kufanya Mshauri awe Mtaalamu tu na siyo mtendaji," anasema.
Nakumbuka maneno yake kwamba, "Mwenyekiti tukiacha kazi hii ifanywe yote na mshauri Mwelekezi, utekelezaji utakuwa mgumu sana kwetu; yeye atakamilisha kazi na atatuachia maripoti tu, kwenye mashelf.” anasema.
Anasema, kiongozi huyo ana sifa ya kubwa ya uwezo wa kusimamia jambo analoliamini kwa maslahi ya wananchi.
“Kwa sababu aliamini kwamba, ni lazima awanu ya pili iongozwe na watanzania, alilisimamia hilo na kuiwezesha serikali kuokoa jumla ya Dola za Marekani 900,000 zilizoweza kuzunguka katika uchumi wa ndani badala ya kulipwa nje ya nchi kwa wataalamu kutoka Peru,” anasema.
Anasema, uwezo wa kufanya maamuzi na kuyatekeleza kwa kasi kuendelea kutekeleza shughuli zake kwa mafanikio.
Anasema, mfano mzuri ni namna urasimishaji wa mashamba ya wakulima wadogo wa chai Njombe ulivyofanyika, kwa uaminifu na uwajibikaji katika kutunza rasilimali za taifa.
Anaongeza kuwa, muda aliokuwepo madarakani kiongozi huyo, kiasi cha fedha kilichokuwa kinapatikana kilikuwa kidogo kuliko mahitaji halisi yaliyo katika mpango kazi.
Hata hivyo, aliweza kusimamia kiasi hicho kidogo na kuweza kufanya kazi kubwa inayoonekana na kukubalika, vinginevyo mpango huo ungeishia awamu ya pili tu.
Anasema, mpango huo unakabiliwa na changamoto kadhaa ukiwamo ukosefu wa fedha ambapo, serikali inafanya jitihada zinazowezekana kuhakikisha fedha zinazohitajika kutekeleza shughuli zilizopangwa zinapatikana kwa wakati.
Anasema, wananchi wana kiu ya kutoka katika umaskini na wanaamini rasilimali walizo nazo na biashara wanazoendesha zina uwezo wa kuwatoa katika hali hiyo.
“Ni wajibu wa MKURABITA kuwasaidia watanzania kupambana na umaskini baada ya kutengewa mazingira mwafaka ikiwamo kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa,” anasema Spika Makinda.
Mratibu aliyechaguliwa hivi karibuni anasema, misingi iliyojegwa mwanzo imeimarisha kitengo na kufanikisha malengo yake katika hatua mbalimbali.
Anamtaja mstaafu huyo kuwa, mtu aliyetumia uwezo wake kuhakikisha malengo ya serikali ya kuleta maisha bora kwa kila mtanzania kupitia urasimishaji rasilimali na biashara yanatimia.
“Tulikuwa tukijiuliza maswali mengi sana ya , ‘Hivi itakuwaje Mzee Salema akistaafu?’ kwa kweli hatukuwa na majibu. Mara nyingine tulithubutu kusema ungekuwa uwezo wetu, ingebidi awepo tu hata akishika mkongojo. Lakini hatukuweza kuzuia.”
Anasema, uwezo aliojenga, utaendelea kutekelezwa na wajibu waliopewa na serikali wa kuwawezesha wananchi kutumia rasilimali na biashara wanazomiliki kuendesha kwa mujibu wa sheria.
Anasema, majukumu ya MKURABITA yanagusa moja kwa moja maisha ya watu ya kila siku hususani wanyonge hivyo, utekelezaji wake unahitaji weledi na uongozi thabiti wenye hekima za kutosha.
Tangia kuanzishwa mpango huo, kwa mujibu wa mratibu huyo, ni kukamilika kwa maandalizi ya maboresho yaliyokuwa msingi wa utekelezaji, na kuendelea na maboresho ambapo jumla ya halmashauri za wilaya 30 na halmashauri za miji 5, zimejengewa uwezo hadi sasa.
Anasema, kwa kushirikiana na Bodi ya Chai na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai, imefanikiwa kurasimisha mashamba ya chai ya wakulima wadogo zaidi ya 400 wa Njombe mkoani Iringa.
Alibainisha kuwa hadi sasa mfumo uliokubalika na unaotumika katika urasimishaji ni ule wa kuzijengea uwezo halmashauri za wilaya na miji ili urasimishaji uongozwe na ufanywe na wao wenyewe katika ngazi za wilaya na miji.
“Hili limewezekana na hivyo, kuiletea MKUTABITA Tuzo ya Umoja wa Mataifa kwa nafasi ya pili Afrika Mwaka 2010 na nafasi ya kwanza mwaka 2011. Tunaamini kwa dhati kabisa kwamba ushindi wa MKURABITA ni ushindi wa Tanzania,” alisema Mratibu huyo.
Ametoa wito kwa kila mtanzania kutambua kuwa anao wajibu wa kipekee wa kupambana na umaskini na hivyo, afanye kila awezalo kumshinda adui huyo.
Kwa upande wake, Eng. Salema anasema, “Unapokuwa na nyumba isiyorasimishwa, thamani yake inakuwa ndogo, lakini ukiirasimisha, inaongezeka thamani na unaweza kuitumia kupata mkopo wa nyumba nyingine na hivyo, ukawa na nyumba mbili huku moja ikilipa deni”
Amewaasa wafanyakazi wa mpango huo, kushirikiana kutoa elimu kwa watanzania kuhusu urasimishaji kwani hadi sasa licha ya malalamiko yaliyopo kwa baadhi ya watu, ukweli ni kwamba uchumi unakua kwa kasi.
No comments:
Post a Comment