13 March 2012

DAWASCO yapania kumaliza vishoka

Na Anneth Kagenda
MAMLAKA ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) imekemea vikali vitendo vinavyofanywa na baadhi ya watu ambao hujifanya wafanyakazi wa mamlaka hiyo na kuwadanyanga watu na kuwaunganishia maji bila kufuata taratibu na sheria jambo linalosababisha kurudisha nyuma juhudi za utoaji huduma hiyo yakiwamo maeneo ya Kibaha na Dar es Salaam.

Pia DAWASCO imesema kutokana na kukidhiri kwa vitendo hivyo wafanyakazi wake watakuwa wakitoa huduma kwa kutoa taarifa katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa husika wakiwa na vitambulisho vya kazi pamoja na kitambulisho cha aina ya kazi aliyoelekezwa kuifanya ili kupunguza wimbi la watu wanaoraghai na kuhujumu.

Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari Dar es Salaam jana, na kusainiwa na Ofisa Uhusiano wa DAWASCO Bi. Teresia Mlengu, ilisema kuwa wananchi hawana budi kuwaepuka watu hao kutokana na kwamba wanakiuka taratibu za utoaji huduma hiyo hivyo kusababisha maeneo mengine kukosa maji.

"Hivi sasa kumeibuka tabia ya watu wasiokuwa wafanyakazi wetu maarufu kama vishoka ambao huwaunganishia huduma ya Maji Safi na Maji Taka wakazi wa Dar es Salaam, Kibaha na Bagamoyo Mkoani Pwani bila kufuata taratibu za utoaji huduma hii kwa jamii," alisema Bi. Mlengu.

Aidha alisema kuwa wananchi wanatakiwa kutambua kuwa kufanyika kwa vitendo hivyo ni kuhujumu mamlaka na pia vinachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma juhudi za Dawasco katika kuhakikisha kila mwananchi anapata maji hayo kwa matumizi sahihi ya mwombaji na kwa gharama zilizoithinishwa na mamlaka husika.

"Wito wetu ni kwamba viongozi wa serikali za mtaa na wananchi wasiruhusu mtu yeyote kulikaribia bomba la DAWASCO katika mtaa wowote bila kufuatwa kwa taratibu tulizoweka," alisema Bi. Mlengu.

Hata hivyo alisema kuwa kuhujumiwa kwa miundombinu ya maji kunahatarisha kukosekana kwa huduma bora ya maji hayo katika mitaa na kusema kuwa wananchi pia hawana budi kuhakikisha wanatoa taarifa ikiwa watawaona watu hao.

"Pia wananchi watusaidie kutoa taarifa kwa watu watakaowaona wakifanya vitendo, wizi wa maji, ukataji wa mabomba, matumizi ya pampu za kuvuta maji, uchepushaji wa dira za maji na uvujaji wa maji katika maeneo husika," alisema.

No comments:

Post a Comment