Na Zahoro Mlanzi
SERIKALI imesema mpaka kufikia mwishoni mwa Aprili mwaka huu Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam utakuwa tayari umekamilika kwa asilimia 75 na utaanza kutumika kwa shughuli mbalimbali rasmi Juni, mwaka huu.
Uwanja huo awali ulitakiwa kukamilika kabla ya sherehe za miaka 50 ya Uhuru lakini mpaka kufikia Desemba 9, mwaka jana ulikuwa haujakamilika, hivyo sherehe hizo kulazimika kufanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Serikali ulisimamisha shughuli za uwanja huo, tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2010/2011.
Akijibu swali kuhusu uwanja huo utakamilika lini, baada ya kushindwa kukamilika kabla ya kuanza kwa sherehe za Uhuru wa miaka 50 Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Leonard Thadeo alisema ni kweli ulitakiwa kukamilika kabla ya sherehe za Uhuru, lakini kikubwa kilichokwamisha ni mkandarasi alichelewesha baadhi ya mambo muhimu.
“Hivi sasa ujenzi unaendelea kama kawaida na ninakuhakikishia mpaka kufikia mwishoni mwa Aprili, mwaka huu utakuwa umekamilika kwa asilimia 75, kwani kazi kubwa iliyobaki ni kuweka viti katika jukwaa mbalimbali zilizojengwa,” alisema Thadeo.
Alisema wakati maboresho hayo yakiendelea kwa kuhakikisha viti vinawekwa na mambo mengine, mpaka kufikia Juni mwaka huu ana imani kila kitu kitakuwa kimekamilika na shughuli mbalimbali zilizokuwa zikifanyika katika uwanja zitaendelea kama kawaida.
Thadeo alisema kukamilika kwa uwanja huo kutapunguza matumizi ya Uwanja wa Taifa, kwani mechi zitakazokuwa si za lazima kuchezewa kwenye uwanja huo, zitafanyika Uwanja wa Uhuru kama ilivyokuwa hapo awali.
Pia alitoa wito kwa mashabiki na wanamichezo kwa ujumla kuhakikisha kuutumia vizuri uwanja huo, pindi utakapokamilika ili kuepusha madhara yatakayoweza kujitokeza kama ilivyokuwa katika mechi ya Kombe la Shirikisho kati ya Simba na Kiyovu ya Rwanda.
Katika mechi hiyo ya Simba, viti 152 viliharibiwa na 11 vilivunjwa kutokana na mashabiki hao kuvunja na kurushiana wakati mechi hiyo ikiwa mapumziko.
No comments:
Post a Comment