09 March 2012

RC awashukia watendaji wenye majungu ofisini

Na Charles Mwakipesile, Mbarali
MKUU wa Mkoa wa Mbeya Bw. Abbas Kandoro, amewataka watumishi wenye tabia ya kuwasema wenzao ofisini 'majungu', kuacha mara moja ambapo watakaobainika kuwa na tabia hiyo, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Bw. Kandoro aliyasema hayo juzi katika hafla ya kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri Wilaya ya Mbaarali, mkoani hapa Bw. George Kagomba.

Hafla hiyo ilifanuyika katika Makao Makuu ya halmashauri hiyo baada ya kustaafu utumishi wa umma na kuongeza kuwa, siri ya mafanikio kwa mtendaji yeyote wa Serikali ni kuchapa kazi kwa bidii, kuepuka majungu.

Alisema kitendo cha kuwagawa wafanyakazi kinakwamisha maendeleo ya wannchi na utekelezaji wa shughuli za Serikali.

“Kiongozi ambaye leo tunamuaga, amefanya kazi kwa bidii na kufanikiwa kuleta mabadiliko makubwa, kufyeka kichaka porini na kujenga Makao Makuu ya Halmashauri.

“Bw. Kagomba ni kielelezo cha watendaji bora wa serikali wasio na majungu  ambaye amewaunganisha wafanyakazi kuwa kitu kimoja na kuharakisha maendeleo,” alisema.


Alisema watendaji wa Serikali ambao wanaendeleza majungu badala ya kufanya kazi, huambulia kufukuzwa na kutokumbukwa kwa lolote walilofanya wakati wa utumishi wao serikalini.

“Sipendi kusikia Mkoa wetu unakosa maendeleo kwa sababu watumishi hutumia muda mwingi kuzungumza habari za majungu badala ya kufanya kazi kwa bidii,” alisema.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Bw. Keneth Ndingo, alisema Bw. Kagomba atakumbukwa kwa mambo mengi pamoja na kujenga Makuu Makuu ya halmashauri hiyo ambayo ina majengo ya kisasa yaliyozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete.

Mbali ya kufanikisha ujenzi wa majengo hayo pia ameweza kukuza pato la halmashauri na ujenzi wa majengo ya sekondari za kata hivyo aliiomba Serikali iangalie uwezekano wa kumuongezea muda wa utumishi kwa mkataba maalumu.

Kwa upande wake, Bw. Kagomba alisema bila kupata ushirikiano kutoka kwa watumishi wengine, asingeweza kufanikisha majukumu aliyopewa ambayo yamezaa matunda.



1 comment:

  1. Yaleyale mtu amestaafu eti anaiomba serikali iangalie uwezekano wa kumuongezea mkataba maalumu!hakuna wengine?hata kama ni bora vipi kuna wengine wanaweza kuwa zaidi yake,sasa hao walio mitaani wafanye kazi gani?tubadilike jamani.

    ReplyDelete