16 March 2012

'Ukomo viti maalum uingizwe Katiba Mpya'

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wanawake ya Chama cha Mapinduzi (UWT), Bi.Sophia Simba amesema suala la ukomo wa ubunge wa viti maalum linatakiwa kuingizwa katika Katiba ya nchi.

Kauli hiyo aliitoa jana wakati akifanya mazungumzo maalum na Majira muda mfupi baada ya kufunga semina elekezi kwa wenyeviti wa UWT wa mikoa, wilaya za Tanzania Bara na Visiwani.

Bi. Simba ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto alisema, jambo la ukomo wa wabunge wa Viti Maalum ni vema likaingizwa katika mchakato wa Katiba Mpya ili kuondokana na kuweweseka kwa wabunge wasiokubaliana na jambo hilo.

Akizungumzia suala la kuwepo kwa ukomo wa nafasi za wabunge wa maalum alisema, wabunge ambao wanaogopa kuwepo kwa ukomo ni wale ambao wanaogopa kuingia majimboni kupigana wenyewe.

Alisema, lengo la kuwepo kwa Viti Maalum ni kuwajengea uwezo wanawake ili nao baada ya muda fulani waweze kusimama wenyewe kugombea ubunge kwa nafasi ya majimbo.

Alisema, inasikitisha kuona kuwa wapo baadhi ya wabunge wa viti maalum ambao hawajui maana ya kuwepo kwa Viti Maalum na kufikia hatua ya kufikiria kuwa watakaa katika nafasi hizo milele.

Hata hivyo alisema, suala la ukomo wa viti maalum haliwezi kuepukika kwani ni mapendekezo ambayo yalitolewa na Baraza Kuu la UWT kwa malengo ya kuwapatia fursa wanawake vijana nao kushika nafasi mbalimbali za uongozi kupitia jumuiya hiyo.

“Nashangaa kuona kuwa wapo baadhi ya wabunge ambao ni wa viti maalumu wakipita mikoani kulalamika kuwa yeye (Sophia) ndiye aliyeleta suala hilo la ukomo wa ubunge wa viti malumu.

“Mimi hiyo siyo hoja yangu ni hoja ya Baraza Kuu la Jumuiya ya Umoja wa Wanawake UWT na hoja hiyo ina malengo mazuri katika kukiboresha chama kwani pasipokuwepo na ukomo wa wabunge, ni wazi kuwa kuna watu ambao kamwe hawawezi kushika nafasi yoyote ndani ya chama,”alisema Bi.Simba.

Bi.Simba alisema anashangazwa na baadhi ya wabunge hao wa Viti Malumu kudai kuwa yeye ndiye amelileta suala hilo katika Baraza kuu la UWT wakati ukweli unajulikana.

Alisema, pamoja na malalamiko hayo bado ukomo ni muhimu kwani unawezesha wengine nao kushika nafasi hizo kupitia viti maalumu.

Mbali na hilo Simba alisema, kama wabunge wa Viti Maalum wataengelea kunag’anga’ania na kukataa kuwepo kwa ukomo ni wazi hakuna haja ya kutaka mfumo wa hamsini kwa hamsini.

Aliendelea kuwarushia makomboa wabunge wenzake ambao ni waviti maalum kuwa wanaopinga ni wale ambao wamekaa katika nafasi hiyo zaidi ya vipindi viwili huku wakiogopa kwenda majimboni kugombea.

“Lakini nataka kurudia kuwa suala la ukomo wa Viti Maalum halikwepeki, kwani kumbuka tumeishaingia mkataba na SADC na Umoja wa Afrika (AU) na mikataba hiyo inaelekeza kuwepo kwa hamsini kwa hamsini sasa iweje wabunge wakawa na kigugumizi cha kukataa ukomo,” alisema Mwenyekiti huyo.

Hata hivyo suala la ukomo wa viti maalum ni la siku nyingi na ndiyo maana baadhi ya wabunge ambao walikuwa wajumbe wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake kama waliamua kugombea nafasi za ubunge majimboni na walio wengi walishinda ubunge.

No comments:

Post a Comment