16 March 2012

NSSF watoa udhamini vipimo vya matibabu

Na Rashid Mkwinda, Mbeya
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limejitolea kudhamini utoaji wa huduma za vipimo kwa wagonjwa wa kisukari na shinikizo la damu kwa wakazi wa wilayani Mbozi ikiwa ni sehemu ya kuhadhimisha wiki ya NSSF kwa mwaka huu.

Huduma hizo za upimaji zimeendeshwa kwa ushirikiano wa Chama cha Madaktari wa Hospitali Binafsi (APHETA) ambapo mamia ya wakazi wa mjini Vwawa walijitokeza kupima afya zao huku wakishauri shughuli kama hiyo iwe endelevu.

Wakizungumza wakati wa upimaji baadhi ya wananchi walisema, shughuli hiyo imehamasisha kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara.

Mmoja wa wakazi wa mjini Vwawa, Bw.Edward Ndisana alisema utaratibu ulioanzishwa na NSSF na APHETA unapaswa kuigwa na mashirika mengine ya serikali na binafsi ambayo yanahusika katika utoaji huduma za kijamii na kwamba wananchi wengi wamekuwa wavivu kupima afya zao kutokana na huduma hizo kuwa mbali na jamii.

Naye Bw.David Sikanyika mkazi wa Tunduma alisema, utaratibu huo utasaidia wananchi kutambua afya zao na hivyo kuchuka hatua ya kujihadhari kutokana na ushauri wa madaktari mara baada ya kupata majibu ya vipimo vya afya zao.

Alisema, amefurahishwa na majibu ambayo ameyapata baada ya kupima na kuwa yatamsaidia kubadili mfumo wa maisha ikiwa ni pamoja na kula aina fulani ya vyakula na nyingine kuviacha na kushiriki mazoezi kila siku.

Kwa upande wake Muuguzi Msaidizi wa Hospitali ya Mbeya Family Care iliyopo Vwawa ,Bi. Agness Msigwa alisema wanatoa huduma ya upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu, kisukari na kupima uwiano wa uzito na urefu na kisha kutoa ushauri.

Akizungumzia ushiriki wa Shirika la Taifa Hifadhi ya Jamii, Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa NSSF, Bi.Theopista Muheta alisema, operesheni hiyo inaendeshwa bure chini ya udhamini wa shirika hilo na kwamba limefanya kwa kuhusisha majiji ya Mbeya, Arusha na Mwanza ambayo kilele chake kinatarajia kufikia Machi 31 mwaka huu.

Alisema, lengo la kuendesha shughuli hiyo ni kusogeza huduma ya tiba karibu na wananchi kwa kutumia huduma zinazotolewa na mfuko huo ambazo hapo awali  zilitolewa kwa wafanyakazi wa mashirika na taasiisi za kiserikali pekee.

Bi.Muheta alifafanua kuwa, uzinduzi wa wiki ya NSSF unatarajiwa kuzinduliwa rasmi leo, katika Jiji la Mbeya na kuwa awali wiki hiyo ilitanguliwa na mashindano ya michezo yanayovishirikisha vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.

No comments:

Post a Comment