FEBRUARI 2009, Rais Jakaya Kikwete alimvua madaraka na kumfukuza kazi aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera, Bw. Albert Mnali, kutokana na kitendo cha kuwacharaza bakora walimu wa shule za msingi wilayani humo.
Hatua hiyo ilitokana na Bw. Mnali kufanya kitendo cha udhalilishaji kisichokubalika katika jamii na kuwavunja moyo walimu.
Bw. Mnali aliamrisha polisi kuwacharaza viboko walimu ambao aliamini wao ndio wamechangia wanafunzi wa shule za msingi wilayani humo kufeli mitihani.
Tukiachana na hilo, wachambuzi wa mambo ya uchumi wanasema ufadhili unaotolewa na wahisani kutoka mataifa mbalimbali duniani una faida na madhara yake.
Mwishoni mwa wiki, gazeti moja linalotoka kila siku liliandika habari inayosema “Mholanzi amchapa vibao Mwalimu Mkuu”. Tukio hili lilitokea katika Shule ya Msingi Marera, iliyopo Kata ya Rhotia, Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha.
Mashuhuda wa tukio hilo wanadai kuwa, raia wa Uholanzi, Bi. Marise Koch, ambaye ndiye mfadhili wa shule hiyo kwa kukarabati majengo ya shule, ofisi, nyumba ya walimu na kutoa kompyuta ndogo 'Laptop', alimdhalilisha Mwalimu Mkuu Bw. Emmanuel Ginwe kwa kumpiga vibao mbele ya wanafunzi, walimu wenzake.
Tukio hilo limeripotiwa katika Kituo cha Polisi Karatu na kufunguliwa jalada namba KRT/RB/835/2012. Bi. Koch aliwakuta walimu wa shule hiyo wakipanga ratiba ya shule na kuhoji kwanini hawajaingia darasani.
Walimu hao walijibu tayari wanafunzi wamepewa kazi za kufanya lakini majibu hayo hayakumridhisha. Aliamua kwenda ofisini kwa Bw. Ginwe na kudai yeye anafadhili vitu vingi lakini walimu hawafundishi, kuanza kukusanya kopyuta alizotoa kama msaada shuleni hapo lakini Mwalimu Mkuu alimsihi asifanye hivyo.
Baada ya Bi. Koch kuona anazuiwa, alimpiga Bw. Ginwe vibao na kuendelea kuzikusanya kitendo ambacho kiliwashtua walimu na wanafunzi walioshuhudia tukio hilo.
Sisi tunasema kuwa, tukio hili halikubaliki kwani dhana ya ufadhili si kunyanyasa watu wanaopewa misaada na kuingiza mambo yao katika mitaala ya elimu nchini.
Kimsingi, kilichofanywa na Bi. Koch ni kosa kisheria hivyo tunaliomba Jeshi la Polisi wilayani Karatu, lichukue hatua stahiki za kuhakikisha mfadhili huyo anafikishwa mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Matatizo yaliyopo katika sekta ya elimu na nyinginezo si kigezo cha kuwafanya Watanzania wanyanyasike na kudhalilishwa ndani ya nchi yao. Tumechoka na manyanyaso ya aina hii, tunataka sheria imuadhibu Bi. Koch kama ilivyofanya kwa Bw. Mnari ambaye alifukuzwa kazi kwa kosa la kudharirisha walimu.
Kama Serikali itashindwa kuchukua hatua stahiki dhidi ya mfadhili huyu, upo uwezekano wa kukwamisha maendeleo ya elimu shuleni hapo kutokana na ukweli kwamba, walimu katika shule husika hawatakuwa na imani na serikali yao kwa sababu haijawali.
No comments:
Post a Comment