Pamela Mollel na Queen Lema, Arusha
RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa, leo anatarajia kuzindua kampeni za mgombea ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha, kwa tiketi Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Sioi Sumari.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa CCM mkoani hapa, Bi. Mary Chatanda, alisema kampeni hizo zitahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho.
Alisema uzinduzi huo utakuwa tofauti na vyama vingine vya siasa ambavyo vinakodisha watu kutoka nje ya jimbo hilo.
“Tutazindua kampeni kwa kishindo ili kuwapa wananchi fursa ya kuona jinsi tulivyojipanga kushinda, kampeni zetu zitafunguliwa na Rais mstaafu, Bw. Benjamin Mkapa na viongozi wengine wa kitaifa watakuwepo ila tumeojipanga kupambana,” alisema Bi. Chatanda.
Katika hatua nyingine, Bi. Chatanda alisema wananchi wanapaswa kutokubali kudanganywa na aina yoyote ya propaganda kuhusu madai ya mgawanyiko wa wanachama ndani ya CCM.
Alisema wanachama wote wapo katika kundi moja jambo ambalo linawapa matumaini ya ushindi. Akizungumzia pingamizi lilowekwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), dhidi ya mgombea wao, Bi. Chatanda alisema pingamizi hilo limefutwa.
Bw. Sumari alikuwa amewekewa pingamizi na CHADEMA kwa madai kuwa hajawahi kukana uraia wa nje.
No comments:
Post a Comment