Na Mkwasi Issa, Pemba
ZAIDI ya miche 15,000 ya mikarafuu inatarajiwa kutolewa kwa wakulima kisiwani Pemba katika kipindi cha mvua za msimu wa masika ambazo zinatarajiwa kuanza kunyesha visiwani humo mwaka huu.
Ofisa wa Mashamba ya Serikali kisiwani Pemba, Bi.Asha Saleh Mbarouk aliyaeleza hayo wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili kuhusiana na mikakati ya Serikali ya kuimarisha zao la karafuu katika msimu huu.
Alisema kuwa, ni vema wakulima kuanza kuyatayarisha mashamba yao mapema kabla ya mvua za masika hazijaanza ili kujiweka tayari kwa ajili ya kupanda mikarafuu mipya.
Bi. Mbarouk alisema, kila mkulima anayehitaji kupatiwa miche ya mikarafuu anatakiwa kujaza fomu ambazo zinapatikana kwa maofisa wa kilimo kwa kila shehia, fomu amabazo zitamuwezesha kupatiwa miche hiyo.
Aidha, alisema miche hiyo inapatikana vitalu vilivyoko Weni katika Wilaya ya Wete, Kicha kwa wilaya ya Micheweni, Kigope Wilaya ya Mkoani pamoja na Kitalu Wilaya ya Chake.
Hata hivyo Ofisa huyo aliwataka wakulima kuwa tayari kwenda kuchukuwa na kujaza fomu ambapo kwa sasa watendaji wa kilimo wameanza kukagua na kupima mashamba operesheni ambayo kwa sasa inaendelea katika shehia ya Mtambwe Kaskazini.
No comments:
Post a Comment