Na Theresia Victor, Dodoma
MHANDISI Deogratius Assey ambaye amejitokeza katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya ubunge, Bunge la Afrika Mashariki (EAC) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amesema tayari amerejesha fomu katika ofisi ya chama hicho mkoani Dodoma kwa ajili ya kugombea nafasi hiyo.
Akizumgumza na Majira baada ya kurudisha fomu hiyo jana, Bw. Assey alisema, alilazimika kuingia katika ushindani huo kwa ajili ya kutaka kutetea maslahi ya vijana kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Bw. Assey alisema, pamoja na kuwepo kwa sera za kuwepo kwa jumuiya hiyo lakini bado haijapata mtu madhubuti ambaye yupo tayari kwa ajili ya kuwatetea na kuwapiagania vijana kuingia katika ushindani wa ajira kupitia EAC.
Alisema, alilazimika kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo kwani alikuwa hajiamini kuwa kama angeweza kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wananchi kwa kumuunga mkono kama ambavyo kwa sasa mambo yamekuwa mazuri kwa kupata ushirikianao wa kutosha.
“Lakini cha kushangaza nimeungwa mkono na wanacha wote wa Chadema na hata wale wasiyo kuwa wanachama, hata hivyo wamenichangia hata gharama za kulipia fomu ambayo ilikuwa inagharimu shilingi laki moja...lakini wamenichangia,”alisema Bw.Assey.
Aliongeza kuwa, ikiwa atafanikiwa kuipata nafasi hiyo atahakikisha kuwa vijana wanatetewa zaidi katika masuala ya ajira tofauti na ilivyo sasa ambapo Watanzania bado hawajaweza kunufaika na suala zima la ajira kwa vijana katika jumuiya.
Aidha, kwa upande wake Katibu wa Mkoa wa Dodoma CHADEMA, Bw. Stivine Masawe alisema, ameipokea fomu ya mgombea huyo na kusema kuwa haina makosa yoyote na hivyo iko sawa na ataiwasilisha Makao Makuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo jijini Dar es Salaam.
Bw. Masawe alisema, kujitokeza kwa Mhandisi Assey ambaye ni kijana na mwanachama hai katika chama hicho ni fursa pekee kwa vijana kutatuliwa matatizo yao kama atapata nafasi ya kuchukua nafasi hiyo ya ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment