Na Elizabeth Mayemba
KOCHA Mkuu wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic amesema hakufurahishwa na matokeo ya suluhu juzi, dhidi ya Toto African ya Mwanza hivyo wachezaji wake wanatakiwa kuvuna pointi tatu kwa Polisi Dodoma kesho. Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Katika mchezo wao uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi timu hizo zilitoka suluhu hivyo kuifanya Simba kukaa kileleni kwa kufikisha pointi 41, sawa na Azam FC tofauti ikiwa kwenye mabao ya kufunga na kufungwa.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, mara baada ya mchezo wao na Toto kumalizika Milovan, alisema matokeo hayakuwa mazuri kwa timu yake pia wachezaji wake waliidharau matokeo yake wakagawana pointi.
"Matokeo si mazuri kabisa, kwani mechi hizi za mwisho ndizo zinazotoa mwelekeo wa nani atakuwa bingwa, hivyo mechi ijayo dhidi ya Polisi Dodoma wachezaji wangu wanatakiwa kuvuna pointi zote tatu," alisema.
Alisema pamoja na beki wake wa kati, Kelvin Yondani kupewa kadi nyekundu nafasi hiyo ataiziba na hakuna pengo kubwa kwa kuwa ana wachezaji wengi wazuri na wanaoimudu nafasi hiyo.
Akizungumzia majeruhi katika kikosi chake, Milovan alisema hali za kiungo wake Mwinyi Kazimoto na beki wa pembeni, Amir Maftah zinaendelea vizuri na wakati wowote wataanza mazoezi mepesi mepesi.
No comments:
Post a Comment