*Apata mapokezi ya kihistoria akitokea Marekani
*Adai Tanzania hakuna utawala wa kidemokrasia
*Wanafunzi 808 Dodoma wakihama chama hicho
Na Peter Mwenda
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amewasili jana akitokea nchini Marekani na kupata mapokezi ya kihistoria.
Wachambuzi wa mambo ya siasa wanasema kuwa, kurejea kwa kiongozi huyo kutasaidia kukinusuru chama hicho ambacho hivi sasa kimekubwa na jinamizi la kuondokewa na wanachama wake.
Profesa Lipumba aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere saa 9:20 alasiri ambapo viongozi mbalimbali wa chama hicho walijitokeza kumpokea wakiwemo wabunge na wanachama wakiongozwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad.
Baada ya kushuka kwenye ndege, Prof. Lipumba alifanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa CUF katika chumba maalumu cha mapumziko.
Baada ya kumaliza mazungumzo, Prof. Lipumba alitoka nje na kuvalishwa shada la maua huku vigelegele na nderemo zikitawala katika maeneo mbalimbali ya uwanja huo.
Eneo la uwaja lilijaa wafuasi wa CUF waliokuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kumpongeza Prof. Lipumba kwa kuwa mwafrika pekee kuchaguliwa kwenye kamati ya kuchunguza chanzo cha mdororo wa uchumi duniani.
Kutokana na wingi wa watu walijitokeza kumpokea, Maofisa Usalama walimzuia Prof. Lipumba na Maalim Seif, kuhutubia wananchi katika uwanja huo.
Maofisa hao walishauri viongozi hao waondoke ndipo Prof. Lipumba aliamua kuzungumza na waadishi wa habari na kusema kuwa, kazi anyoifanya nchini Marekani angeweza kuifanya Tanzania kama mchumi aliyebobea lakini hapati ushirikiano.
“Nipo tayari kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania kuhusu masuala ya uchumi, hii itatokana na utawala na demokrasia ambao kwa sasa haupo nchini Tanzania,” alisema.
Aliwashukuru Watanzania na wafuasi wa CUF kwa kujitokeza kumpokea na kudhihilisha kuwa, wananchi wana imani na chama hicho.
Kwa upande wake, Shekhe Issa Ponda, akiongoza mashekhe wenzake 20 kutoka misikiti mbalimbali jijini Dar es Salaam, alisema mchango wa Prof. Lipumba ni heshima kubwa kwa Tanzania.
Ofisa Mawasiliano wa CUF, Bw. Salium Biman, alisema chama hicho kitachukua dola mwaka 2015 kutokana na umati mkubwa wa watu waliojitokeza uwanjani wenye imani na Prof. Lipumba.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu CUF Zanzibar, Bw. Ismail Jussa Ladhu, alisema umati uliojitokeza kumlaki Mwenyekiti huyo ni salamu tosha kwa mbunge wa Wawi, Bw. Hamad Rashid Mohammed kuwa chama hicho bado kina nguvu.
“CUF imeanza kazi rasmi ya kuimarisha chama ili 2015 tuchukue dola kwa kishindo,” alisema, Bw. Jussa.
Baada ya kuzungumza na waandishi wa habari, Prof. Lipumba aliondoka na msafari wa watu walifika kumpokea ukiongozwa na pikipiki, magari na watembea kwa miguu hadi Uwanja wa Karume.
Awali mapokezi hayo yaliingia dosari baada ya gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T 854 AMN, lililokuwa limejaza wafuasi wa chama hicho, kupinduka na kusababisha watu 10 kuumia.
Taarifa nyingine zinasema kuwa, gari lingine ambalo lilikuwa likitokea Rufiji mkoani Pwani kupeleka wafuasi wa chama hicho uwanjani hapo, lilimgonga mtembea kwa miguu na kufa papo hapo.
Wakati huo huo, Mwandishi wetu kutoka Dodoma anaripoti kuwa, zaidi ya wanafunzi 808 wa Vyuo Vikuu mkoani hapa ambao ni wananchama wa CUF, wametoa tamko la kujitoa na kurudisha kadi kwa uongozi wa chama hicho kwenye matawi ya vyuo vyao.
Wanafunzi hao walidai kuwa, wamelazimika kujiondoa katika chama hicho kutokana na kitendo cha viongozi wa ngazi ya juu kujali zaidi maslahi binafsi na kukidumaza chama.
Tamko la kujitoa katika chama limetolewa na Mwenyekiti wa Tawi la St. John Bw. Muhamed Abdullha kwa niaba ya wanafunzi wezake katika kikao kifupi kilichofanyika kwenye Ukumbi wa mikutano chuoni hapo.
Bw. Abdullah alisema wanachama waliojitoa ni wasomi wa elimu ya juu katika vyuo vyote mkoani haapa ambao wamerudisha kadi za chama hicho na kila mmoja atachagua chama cha kwenda ambacho kina mtazamo wa kuleta maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
“Uongozi wa CUF kimsingi umetuchosha, hatujui unajali maslahi ya nani, inaonesha wazi kuwa viongozi wachache wa juu wanalinda maslahi binafsi na ndiyo maana chama hakikui.
“Kutokana na hali hiyo, wanafunzi ambao ni wanachana wa CUF tumelazimika kurudisha kadi, kila mmoja atachagua cham cha kwenda chenye mwelekeo wa kusaidia wananchi,” alisema.
Walisema Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Bw. Ismail Jussa Ladhu, amekuwa akitumia madaraka yake vibaya na kukiuka katiba ya chama hicho jambo ambalo limekuwa kilichangia kuwepo matakaba kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Katika tamko lao, wanafunzi hao walidai kuchoshwa na tabia za viongozi wa chama kuingiza udini kwa kuwabagua Wakristo na Waislamu na kujenga ukuta kati ya Wazanzibari na wenzao wa bara jambo ambalo ni kinyume na katiba yao.
hao wanafunzi ni wanafik hawana subra wala hawajui wanataka nini wanadandia tuu mwanacham wa kweli wa Cuf hatoki washanunuliwa na hao MMungu Mkubwa atakilinda chama na inshallah atikipa ushindi na neema itakuja kwa uwezo wake Muumba kwani CUF kinaomba dua kila aliye mnafik atoke kwenye chama ili tupate wanacha wa kweli wasionunulika ama kwa fedha wala kwa mawazo. sihija kuwa ni wasomi kinachotakiwa kwa msomi ni kutumia akili zaidi na sio utashi sasa wao wanatumia utashi na mapenzi kwa mtu fulani
ReplyDeleteNinasikitika kuwa habari zote picha zake zimewekwa ila hii ya mapokezi ya Mheshimiwa lipumba haijaweka tuseme nafasi ilikuwa hakuna au vipi.
ReplyDelete