*Wadaiwa kumpiga mtoto, mechi yao yaingiza mil. 73/-
Na Zahoro Mlanzi
WACHEZAJI wa Yanga Nurdin Bakari, Athuman Idd 'Chuji' na Jerryson Tegete, wanadaiwa kumpiga mtoto anayeishi Mtaa wa Faru na Swahili, Kariakoo, Dar es Salaam na kumsababishia maumivu.
Tukio hilo lilitokea juzi usiku baada ya mtoto huyo kuwazomea kutokana na kipigo cha bao 3-1 dhidi ya Azam FC ambapo gari la Yanga lililokuwa limebeba wachezaji, lilisimama na wachezaji hao kwenda kumpiga mtoto huyo ngumi na mateka.
Kwa mujibu wa shuhuda aliyekuwepo eneo la tukio (jina tunalo), alisema “ Baada ya mtoto huyu kuwazomea, Chuji, Nurdin na Tegete walishuka kwenye gari la kumuadhibu, walipomaliza kiu yao walirudi katika basi lao na kuondoka,” alidai mtoa habari huyo.
Alidai kuwa, walipokwenda kumuangalia mtoto huyo walimkuta katika hali mbaya huku mwili wake ukiwa na majeraha.
Vyanzo mbalimbali vya kuaminika vilidai kuwa, mtoto huyo alikimbizwa hospitali kutokana na hali yake kuwa mbaya.
Alipotafutwa kwa njia ya simu ili aweze kuzungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda Mkoa wa Kipolisi Ilala, Saada Juma, alisema hana taarifa zozote kwani hadi anaondoka ofisini juzi saa 1:30 usiku, hakuna mtu aliyetoa taarifa ya tukio hilo.
“Leo (jana) Ma-OCD wangu walikuwa wakinipa taarifa za mara kwa mara kuhusiana na tukio la kuwasili kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Ibrahim Lipumba lakini taarifa za kupigwa mtoto hadi akafariki dunia au kukamatwa kwa wachezaji wa Yanga hilo sijalipata,” alisema Kamanda Juma.
“Kama lipo nadhani nitapata taarifa ila kinachonishangaza, tutaanzaje kupaata taarifa za kifo kabla ya kuumizwa mtoto husika kwani hizo ndio zingesaidia kupata majibu ya uhakika kwa hicho unachonieleza lakini siwezi kusema uongo ila ukweli ni kwamba sina taarifa na hilo,” alisema.
Majira halikuishia hapo pia lilimtafuta Mwenyekiti wa klabu hiyo, Llody Nchunga ambaye alisema hana taarifa za wachezaji wake kufanya fujo, kukamatwa au kufa kwa mtoto huyo.
“Sijui kama hilo tukio lina ukweli, ninachokiamini mimi ni kwamba, wachezaji wote walirudi klabuni na leo (jana) asubuhi, nilikwenda kuzungumza nao tukaamua kuwapa siku moja ya mapumziko hivyo wamekwenda majumbani kwao,” alisema Nchunga.
Alisema kama tukio hilo lilifanyika, labda ni baada ya kurudi klabuni na baadhi yao kutoka tena kwenda mitaani kufanya fujo lakini walipotoka uwanjani, warurudi klabuni.
Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu timu hiyo, Kostadin Papic atawachukulia hatua wachezaji wote waliomfanyia fujo mwamuzi Israel Mujuni kutoka Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Papic alisema kitendo kilichofanywa na wachezaji wake hakikuwa kizuri na utovu wa nidhamu hivyo atahakikisha anawachukulia hatua.
Wakati huo huo, mchezo kati ya Yanga na Azam umeingiza sh. milioni 72,731,000.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari Dar es Salaam na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema watazamaji 19,339 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 3,000 viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B wakati kwa VIP A ilikuwa sh. 15,000.
No comments:
Post a Comment