*Ataka mafisadi watoswe katika chaguzi za chama hicho
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Samuel Sitta, amewapa mtihani mzito wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Mwanza na mikoa mingine nchini kuweka historia katika chaguzi mbalimbali ndani ya chama hicho kwa kukisaficha chama na kuwatosa wagombea wanaotaka uongozi kwa maslahi binafsi kwani wanachangia kukishushia hadhi chama hicho.
Alisema kama mafisadi na makundi yao yatapewa nafasi za uongozi ndani ya chama, watajuta kupoteza nafasi muhimu ambazo zinapaswa kufanyiwa mabadiliko ya kihistoria na watakuwa wameshiriki kuisaliti CCM na kuiweka pabaya chaguzi zijazo.
Bw. Sitta aliyasema hayo juzi katika mkutano wa hadhara ambao ulihudhuriwa na maelfu ya wana CCM pamoja na waananchi katika Uwanja wa Magomeni, uliopo Kata ya Kilumba, jijini Mwanza.
Alisema njia pekee ya kuinusuru CCM ni wanachama kuhakikisha wanachagua viongozi waadilifu kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa.
Aliongeza kuwa, wananchi wengi bado wana imani na chama hicho lakini wanalalamikia mwenendo wa baadhi ya viongozi hivyo uchaguzi wa mwaka huu lazima uwe wa kihistoria.
“Hii ndio fursa ya kukinga’risha chama chaetu, wana CCM tumieni uchaguzi huu kuchagua viongozi wanaopinga aina zote za ubaguzi ukiwemo wa kipato, tuchague viongzoi wenye huruma na wanaotetea wanyonge ambao ndio wengi.
“Tusipofanya hivyo na kuwaachia wenye uchu na matajiri, tutakuwa hatujaitendea haki imani yetu, itikadi yetu na misingi yetu, tuweke historia katika uchaguzi huu kwa kuwaenzi waasisi wetu wa Taifa.
“Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alituachia msingi wa CCM kutetea wanyonge na huu umedhihirika, tumekuwa wakombozi hadi nje ya nchi, ukombozi huo ndio aliomnfanya Mzee wetu Karume kuwajengea maghorofa wanyonge hivyo lazima turudi katika misingi hiyo,” alisema Bw. Sitta.
Bw. Sitta ambaye alialikwa na Kamati ya Siasa Wilaya ya Ilemela na Kata ya Kirumba kuzindua kampeni za kumnadi mgombea udiwani wa kata hiyo, alisema CCM imekuwa ikilaumiwa na Watanzania kwa kupoteza uelekeo, kushindwa kuendeleza sera na itikadi iliyomo ndani ya katiba yake.
“Imani yetu rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa, huu ndio wakati wa kurudisha chama chetu katika njia yake na kusafisha vumbi la kila aina ili CCM ing'ae mbele ya jamii, tusipofanya hivyo, tutakua hatukitakii mema,” alisema.
Akimnadi mgombea udiwani wa kata hiyo, Bw. Jackson Robert, maarufu kama 'Masamaki', Bw. Sitta alisema mgombea huyo anastahili kuchaguliwa kutokana na uadilifu na msimamo wake thabiti katika kusimamia sera za CCM.
Alisema ushindi alioupata wa asilimia 70 ndani ya chama hicho ni dalili ya ushindi wake katika uchaguzi huo.
Bw. Robert atachuana wagombea wengine wa vyama mbalimbali huku mpinzani wake mkuu akitarajiwa kutoka chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
No comments:
Post a Comment