15 March 2012

Mafisango azidi kuipaisha Simba

*Yanga nayo yatakata U/Taifa
Na Pendo Mtibuche, Dodoma

KIUNGO wa Simba, Patrick Mafisango jana alizidi kuipasha timu hiyo katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuifungia timu bao la ushindi dhidi ya Polisi Dodoma katika mchezo huo uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.

Kwa matokeo hayo, Simba inaendelea kuonza ligi hiyo kutokana na kuwa na pointi 44, ikifuatiwa na Azam FC huku Yanga ikishika nafasi ya tatu.

Mechi hiyo ilianza kwa kasi huku kila timu ikitaka kufunga bao lakini hata hivyo, mabeki wa kila upande walikaa imara kuondoa hatari zote.

Simba ilipata bao dakika ya 46 kupitia kwa kiungo wake, Patrick Mafisango.

Kipindi cha pili Simba ilicharuka ambapo washambuliaji wake, Felix Sunzu na Emmanuel Okwi walikuwa mwiba kwa mabeki wa Polisi Dodoma kutokana na kasi yao.

Washambuliaji hao waliweza kushirikiana vyema katika safu ya ushambuliaji, lakini hata hivyo mabeki wa Polisi walikaa imara kuwabana wasilete madhara.

Dakika ya 80, Salum Machaku wa Simba alizawadiwa kadi ya njano kutokana na kumchezea mchezaji mmoja wa Polisi.

Naye Zahoro Mlanzi, anaripoti kuwa mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga jana waliondoka na pointi tatu katika mechi ya Ligi Kuu iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kuifunga African Lyon bao 1-0.

Kwa matokeo hayo, Yanga imefikisha pointi 40 huku ikiendelea kuzifukuza Simba inayoongoza ligi hiyo, ambayo inafuatiwa na Azam FC yenye pointi 41.

Yanga ndiyo ilianza kupata bao dakika ya 43, lililowekwa kimiani na Kigi Makasy baada ya kukutana na mpira uliopigwa fyongo na beki, Yusuf Hamis akiwa katika harakati ya kuokoa.

Katika mechi hiyo African Lyon ilianza kwa kukamia ikitaka kufunga mabao, licha ya mpira kupooza dakika za mwanzo.

Dakika ya 15 Davies Mwape, nusura aifungie Yanga bao kwa kichwa akiunganisha krosi ya Keneth Asamoah.

Mwape alikosa bao lingine dakika 16 baada ya kubaki na kipa wa Lyon, Abdul Seif akiwa ameutokea mpira uliochongwa na Shamte Ally, lakini hata hivyo kipa huyo akaokoa hatari hiyo na kuwa kona tasa.

Baada ya kosakosa hizo, African Lyon ilizinduka na kuanza kuisumbua ngome ya Yanga, ambapo dakika ya 22 Benedict Kaguo, aliachia shuti lililotoka nje kidogo ya lango akiwa amepokea pasi ya Hood Mayanga.

Dakika ya 27, Mayanga uliopigwa mbali na kubaki yeye na kipa Said Mohamed wa Yanga, lakini shuti lake likatoka nje kidogo ya lango.

Kipindi cha pili Yanga, iliwatoa Mwape na Kigi Makasy na nafasi zao kuchukuliwa na Pius Kisambale na Idrisa Rashid.

Katika kipindi hicho, timu zote zilishambuliana kwa zamu huku Yanga ikitaka kuongeza la pili na African Lyon ikitaka kusawazisha.

Dakika 86 Kisambale alishindwa kuifungia timu yake bao baada ya kupokea pasi ya Shedrack Nsajigwa, lakini shuti lake likaokolewa na kipa wa Lyon.

ends......


No comments:

Post a Comment