*Wamwambia asiogope gereza kwa kutetea wananchi
Na Queen Lema, Arumeru
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemtaka mgombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mdogo Jimbo la Arumeru Mashariki, Bw. Joshua Nasari, kuwa jasiri na kutoogopa kwenda gerezani kwa kutetea haki za wananchi.
Meneja kampeni wa chama hicho katika uchaguzi huo, Bw. Vicent Nyerere, ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Mjini, aliyasema hayo jana wakati akimnadi Bw. Nassari katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye eneo la Songoro Sura.
Alisema wabunge wa chama hicho si waoga wa kushtakiwa wala kwenda gerezani kwa kutetea haki za wananchi waliowachagua hivyo ni wajibu wake kutekeleza hilo kwa kusimamia haki zao.
“Hakikisha anatenda haki na kuwa jasiri, usiogope kwenda gerezani na kama utashindwa kusimamia haki, tutamsimamisha mgombea mwingine hivyo onesha ujasiri,” alisema Bw. Nyerere.
Alisema CHADEMA haiitaji mtu ambaye si jasiri asiyeweza kusimamia ukweli na kutekeleza sera za chama.
Kwa upande wake, Mbunge wa Karatu kwa tiketi ya chama hicho, Mchungaji Israel Natse, alisema wananchi bila kujali itikadi zao wanapaswa kulinda amani iliyopo na yule ambaye itabainika anasababisha vurugu, chama hicho kitamkamata.
“Mtu yeyote ambaye atafanya fujo katika uchaguzi hata kama atavaa nguo za chama tutamkamata, wapo vaadhi ya wapinzani wetu ambao ambao huvaa nguo zetu ili kutuharibia, hatuwezi kukubali,” alisema.
Kwa upange wake, Bw. Nassari aliwaomba wananchi wamchague kwa kumpa kura nyingi ili aweze kutatua matatizo yao ambayo yamedumu muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment