13 March 2012

Arumeru msitumie vibaya haki yenu

KUANZIA juzi vyama vya siasa vimeanza kampeni ya kuwania ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ndio kilichoanza kufungua pazia la kampeni ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimefanya uzinduzi wake jana.

Sisi tunaamini kuwa, vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huu vitatumia fursa hiyo kunadi sera badala ya kutumia lugha isiyokubalika kwenye jamii kama ilivyotokea chaguzi zilizopita.

Kama vyama vyote vitazingatia umuhimu wa kunadi sera zao, itakuwa fursa nzuri kwa wananchi kuchagua chama ambacho kitawapatia ufumbuzi wa matatizo yao.

Tunaamini kuwa, uchaguzi wa Arumeru Mashariki ni kipimo cha namna wananchi wanavyoridhika na watawala walio madarakani.

Wilaya hii inakabiliwa na migogoro mingi ya ardhi ambayo imeshikwa na matajiri wanaojihusisha na kilimo cha maua ambacho kinaingiza fedha nyingi za kigeni.

Pamoja na faida kubwa zitokanazo na kilimo hicho, wananchi wanalalamika kutonufaika na uwekezaji huo. Wafanyakazi waliopo katika mashamba husika, wanalalamikia malipo duni yasiyolingana na kazi wanayofanya.

Tunahitaji kwenye kampeni hizi, tusikie wagombea wakitueleza namna watakavyoweza kutatua tatizo hilo. Tunasema hivyo kwa sababu, uwekezaji usiokuwa na faida ndiyo unawafanya wananchi waichukie Serikali yao.

Kwa msingi huo, tunaamini hasira hiyo itahamishiwa katika sanduku la kura ili kumpata mbunge ambaye atasimamia haya kwa uadilifu mkubwa kwani hakuna sababu ya wakazi wa Wilaya hii kuendelea kubaki nyuma.

Tunataka wagombea watueleze mikakati yao katika kushughulikia changamoto husika na kuzipatia ufumbuzi katika muda mfupi.

Changamoto nyingine kubwa kwa wakazi wa Meru ni haki ya kupata maji. Meru kuna maji mengi lakini matajiri wenye mashamba wameyazuia hivyo wananchi wa kawaida hawapati.

Ipo tabia ya baadhi ya wagombea wanaotoa fedha kwa wananchi ili wachaguliwe. Tabia hii imeanza kujionesha kwa vyama mbalimbali hasa vyenye wabunge.

Kwa hali ilivyo sasa 'ni rashisi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko maskini kupata uongozi ndani ya CCM, mwenye kisu kikali kwenye chaguzi ndiye anayekula nyama.'

Vyama vyote vya siasa vinatambua hili lakini hawajui pa kutokea. Jambo hili ndilo limeifikisha nchi yetu pabaya kwa kuwa na viongozi wenye malengo binafsi.


Matajiri wanatafuta uongozi ili walinde biashara zao. Wengine wanakimbilia ubunge kusaka mitaji. Choche wakazi wa Meru chagueni kiongozi mwenye uwezo na sifa za kuwatumikia.

  



No comments:

Post a Comment