16 February 2012

Yanga yapata 'dawa' ya walunguzi tiketi

Na Zahoro Mlanzi

KATIKA kuhakikisha wanadhibiti ulanguzi uliopo kwenye uuzaji wa tiketi, Klabu ya Yanga kwa kushirikiana na Kampuni ya Prime Time Promotions, zitatumia kifaa maalumu kitakachotumia kompyuta kukagulia tiketi wakati wa mechi yao dhidi ya Zamalek ya Misri, itakayopigwa Jumamosi Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Mbali na kutangaza mpango huo, pia wameweka wazi viingilio vitakavyotumika katika mechi hiyo kwamba cha juu ni sh. 50,000 na cha chini ni sh. 3,000.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa pambano hilo ambaye ni mwakilishi kutoka Prime na Cloud's Media, Balozi Kalamba alisema kwa kushirikiana na Yanga, wameandaa utaratibu mpya wa kuingia uwanjani.

"Katika kuhakikisha tunadhibiti wimbi la wizi wa tiketi, tumeamua tuwe na tiketi ambazo huwezi kuingia uwanjani mpaka zikaguliwe kwa mashine ambayo itakuwa ikiongozwa na kompyuta.

"Siku hiyo kutakuwa na kompyuta zaidi ya 10 uwanjani, ambazo zitagawanywa katika mageti mbalimbali ya kuingilia, hivyo tiketi ikishahakikiwa na kifaa hicho ukiirudia tena itajulikana," alisema.

Alisema pia kifaa hicho kitasaidia kujua ni watu wangapi waliopo uwanjani, wakati mechi ikiendelea kuchezwa hivyo itasaidia hata kujua ni mapato kiasi gani yamepatikana.

Alishauri kwa wapenzi wa soka nchini kununua tiketi mapema na kuingia mapema uwanjani, ili kupunguza msongamano wakati wa kuingia.

Naye Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa alisema kwa mujibu wa Kocha Mkuu Kostadin Papic, timu hiyo inaendelea vizuri na mazoezi na mpaka sasa wana majeruhi Salum Telela na Nurdin Bakari pekee.

Alisema tiketi zitaanza kuuzwa leo katika vituo mbalimbali na kwamba kiingilio kwa Viti Maalum A ni sh. 50,000, VIP B sh. 30,000, VIP C sh. 15,000, viti vya machungwa sh. 10,000, viti vya bluu sh. 7,000 na kijani sh. 3,000.

Aliongeza kuwa wapinzani wao watatua nchini kesho alfajiri na jioni wanatarajia kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa.

Wakati huohuo, Mwesigwa aliongeza kuwa timu yake kwa sasa imeondoka Makao Makuu ya klabu hiyo, Mitaa ya Twiga na Jangwani na kwamba wameamua kuiweka mafichoni.








No comments:

Post a Comment