16 February 2012

TBL yajitosa Miss Tanzania kwa mil. 700/-

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha Redd's Original jana imetangaza rasmi kudhamini mashindano ya Miss Tanzania kwa sh. milioni 700 kwa mwaka huu.

TBL ambayo imechukua mikoba ya Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom, imeingia mkataba wa miaka mitatu na Kamati ya Miss Tanzania kuanzia mwaka huu hadi 2014. 

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es salaam jana, Meneja Masoko wa TBL, Fimbo Butallah alisema baada ya kampuni yake kuwa mdhamini mkuu wa mashindano hayo, sasa yatajulikana kwa jina la Redd's Miss Tanzania.

"Kwa miaka kadhaa sasa Redds Original, imekuwa ikishiriki katika mashindano haya kama mdhamini mwenza, yaani “kinywaji rasmi cha Miss Tanzania.”

"Hivyo leo tunapiga hatua nyingine kubwa katika historia ya tasnia hii ya urembo hapa nchini kwa kuwa mdhamini mkuu wa mashindano ya Miss Tanzania," alisema Butallah.

Alisema katika kuonesha kuwa Redd's Original, imedhamiria kwa dhati kuendeleza tasnia ya urembo ndiyo maana jana wakasaini mkataba wa udhamini wa mashindano haya kwa kipindi cha miaka mitatu.

Alisema kusaini mkataba wa miaka mitatu itawahakikishia wapenzi na mashabiki wa Miss Tanzania kuwa wataendelea kushuhudia mashindano hayo na kuburudika na kinywaji cha Redds Original kwa kipindi chote hiki.

Naye Meneja wa Redds Original, Victoria Kimaro alisisitiza juu ya udhamini wa mashindano hayo kuanzia ngazi za chini hadi taifa.

"Tunawaahidi mashabiki wote wa mashindano haya na wadau wa tasnia ya urembo kujiandaa kwa burudani ya hali ya juu," alisema.

Akizungumzia udhamini huo, Mkurugenzi wa Lino International Agency ambao ndiyo waandaaji wa Miss Tanzania, Hashim Lundenga alitoa shukurani kwa TBL kwa udhamini huu, na wanakubaliana na wadhamini hao kwamba kuanzia sasa mashindano hayo yatakuwa yakiitwa Redds Miss Tanzania.

"Kitu kikubwa tunachowashukuru wadhamini wetu ni mkataba ambao tumesaini hii leo, (jana) ukituhakikishia udhamini wa mashindano haya kwa miaka mitatu.


No comments:

Post a Comment