Na Speciroza Joseph
TIMU ya Azam FC, imezidi kuzifukuza Simba na Yanga katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, baada ya kuishushia kipondo Villa Squad cha mabao 4-1 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo wa jana, Azam imefikisha pointi 36 nyuma ya vianara Simba yenye pointi 37 sawa na Yanga ila zinatofautiana kwa bao moja.
Katika mechi hiyo, Villa ndio walikuwa wa kwanza kubisha hodi lango mwa Azam na dakika ya 21, Nsa Job aliifungia timu yake bao kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Ahmed Salum.
Kutokana na kufungwa bao hilo, Azam ilitulia na kusawazisha dakika ya 26 kupitia kwa Salum Abubakari aliyepiga shuti la mbali na kutinga moja kwa moja wavuni na dakika mbili baadaye Abdi Kassim alifunga bao la pili.
Dakika ya 43, Azam walifunga bao la tatu kupitia kwa Khamis Mcha akiunganisha krosi ya Kipre Tchetche na dakika mbili baadaye Tchetche alifunga bao la nne la kufanya mpaka mapumziko Azam kuongoza kwa mabao 4-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na dakika kati ya 49 mpaka 52, mchezo ulisimama kutokana na mashabiki wa Villa kurusha chupa uwanjani baada ya Joseph Mahundi kufunga bao lakini Mwamuzi Msaidizi, Pili Abdallah kulikataa akidai ameotea.
Baada ya tukio hilo, mechi iliendelea lakini wachezaji wa timu zote walionekana kucheza kwa kukamiana na kufanya mchezo kukosa ladha kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza.
Mpaka kipyenga cha mwisho kikipulizwa Azam waliibuka na ushindi wa mabao 4-1.
No comments:
Post a Comment