16 February 2012

Wanafunzi 30 wanachama wa 'Al-Shabaab' wasimamishwa

John Gagarini, Kibaha

WANAFUNZI 30 wanaodaiwa kuanzisha vikundi vya Al-Qaeda na Al-Shabaab katika Shule ya Sekondari ya Kata Mwanalugali, iliyopo Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani, wamesimamishwa masomo hadi Bodi ya Shule itakapoamua vinginevyo.

Uamuzi huo ulifikiwa jana shuleni hapo katika mkutano wa walimu na wazazi wa wanafunzi wanaosoma shule hiyo.

Katika mkutano huo, wazazi walishinikiza kwa kauli moja wanafunzi hao kusimamishwa masomo baada ya mmoja wao ambaye ni mwanachama wa kundi mojawapo, Rajab Mohamed, kumpiga na kumvunja jino mwalimu wake Bw.Lazaro Sule.

Wanafunzi waliofukuzwa ni wa kidato cha pili na tatu ambapo wazazi wenye watoto, walikabidhiwa barua za kusimamishwa masomo ili kutoa nafasi ya kufanyika uchunguzi.

Katika uchunguzi huo, wanafunzi ambao itabainika kuwa chanzo cha vurugu shuleni hapo, watachukuliwa hatua zaidi na wale ambao watanusurika, wataruhusiwa kuendelea na masomo.

Miongoni mwa wazazi hao, Bi. Dina Koya, alisema wanafunzi hao wametia doa shule hiyo kwa kufanya vitendo ambavyo haviwezi kuvumilika kwani wanatia hofu hata kwa wananchi wa kawaida.

“Wengine wanajihusisha na vitendo vya uvutaji bangi na hutumia mapanga kufanya vurugu, hii shule tumeijenga wenyewe kwa kutoa eneo na tumebeba vifusi vya udongo, leo hii baadhi ya wanafunzi wanafanya ionekane haina maana, kimsingi hatuwezi kukubali ni heri waondoke, watatuharibia shule yetu,” alisema mzazi mwingine Bw.Ally Maandiko.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Bw. Aron Ndunguru, alisema lengo la kusimamishwa wanafunzi hao ni kupisha uchunguzi juu ya vikundi hivyo.

Wanafunzi wa kidato cha tatu ambao wanadaiwa kuunda kikundi cha Al-Qaida ni Mandela Ibrahim, Kibabu Majid, Mbaraka Said, Kelvin Michael, Daniel Alfonce, Rajab Mohamed, Makame Shaban, Khalifa Rashid, Mohamed Abdu, Simon John, Pascal Emanuel, Elizabeth Yusuph, Fausta Michael, Zakia Rashid na Sikudhan Juma.

Wengine wanaounda kundi la Al-Shabaab ambao ni wanafunzi wa kidato cha pili ni Shakila Mohamed, Caroline Hillary, Zainab Dokodoko, Issa Jumanne, Abel Nambala, Shaban Rajab, Michael Mhilu, Bafana Suta, Clinton Stanford, John Peter, Shaban Siraji, Nasoro Ally, Raymond Stephen na Maimuna Abel.

3 comments:

  1. Jossey: Tusipojihadhari itakuwa kama Boko Haram, kwani nao walianza mchezo kama huo, hao wanafunzi wasionewe haya hatua zichukuliwe za kutosha,

    ReplyDelete
  2. Wakati mwingine mambo mazito huanza kimzahamzaha, lakini matokeo yake ndio huwa majuto.
    Hawa vijana wanafanya mzaha na mambo mazito kutokana na kukosa ufahamu. Nadhani wanakosa elimu ya kuwafahamisha vikundi hivyo wanavyovishabikia vina shabaha zipi. Maskini hawa, kwanza wapo shule ya kata, halafu wanafanya mchezo wa balaa hili.
    Wazazi, hawa wanenu mtawapoteza, kwani hawajui hatari zinazotokana na mchezo huu hatari.

    ReplyDelete
  3. BUNDALA SHIWALA EMMASMay 21, 2012 at 1:31 PM

    KWA WALE WATAKAOONEKANA WANAWEZA KUENDELEA NA MASOMO,NI BORA WATAWANYWE WASIWEKWE TENA SHULE MOJA.

    ReplyDelete